2012-11-12 08:51:53

Baraza la Makanisa Ulimwenguni lampongeza Askofu mkuu mteule Justin Welby


Dr. Olav Fyskse Tveit, Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni, amemwandikia salam na matashi mema, Askofu mkuu mteule Justin Welby wa Jimbo la Durham, Kanisa Anglikana kwa kuteuliwa kwake kuwa kiongozi mkuu wa Jumuiya Waanglikani Duniani. Anakumbusha kwamba, Kanisa Anglikani ni kati ya wanachama waasisi wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni.

Askofu mkuu mteule anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Askofu mkuu Rowan Williams wa Cantebury ambaye anang’atuka madarakani na anatarajiwa kufundisha Chuo Kikuu cha Cambridge, kilichoko Uingereza.

Katibu mkuu kwa niaba ya Baraza la Makanisa Ulimwenguni anapenda kuchukua fursa hii kumkaribisha kwa kutambua mchango wa Kanisa Anglikani katika jitihada za majadiliano ya kiekumene na kwamba, wanatarajia kujenga na kuimarisha zaidi umoja miongoni mwa Makanisa haya. Dr. Tveit anasema, anatambua mchango mkubwa ambao Kanisa Anglikani linaendelea kutoa kwa ajili ya maisha na ustawi wa Kanisa na wananchi wa Nigeria katika ujumla wao.

Mwelekeo huu unaoneshwa pia na Askofu mkuu mteule Justin Welby, hasa kwa kutaka kuwasaidia wananchi wa Nigeria kuvuka vikwazo vya mashambulizi ya kigaidi pamoja na kujenga mshikamano wa dhati kati ya waamini wa dini ya Kiislam na Kikristo nchini humo, kwa njia ya majadiliano ya kidini yanayopania mafao ya wengi.

Hili ni jukumu ambalo Baraza la Makanisa Ulimwenguni linapania kuliendeleza katika siku za hivi karibuni nchini Nigeria. Ni matumaini ya Baraza hili kwamba, Askofu mkuu mteule, ataunga mkono jitihada hizi kwa ajili ya mafao ya wengi nchini Nigeria na kwamba, atakuwa ni kiongozi wa Kanisa kwa sasa na kwa siku zijazo.

Dr. Olav Tveit anamshukuru kwa namna ya pekee, Askofu mkuu Rowan Williams kutokana na mchango wake mkubwa katika maisha na utume wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni uliosimikwa katika urafiki wa dhati. Ni matumaini yake kuwa wataendeleza urafiki huu hata kwa siku za usoni.









All the contents on this site are copyrighted ©.