2012-11-10 07:42:30

Waraka wa Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya kuelekea Uchaguzi Mkuu nchini humo


Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, linasema, mwanzo kabisa wa maadhimisho ya Mwaka wa Imani uliofunguliwa hivi karibuni na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, na utakaohitimishwa hapo tarehe 24 Novemba 2013, Mama Kanisa anawaalika waamini kwa namna ya pekee, kutubu na kuongoka, ili waweze kuwa karibu na Kristo, kwa kuishi kikamilifu Ukristo wao katika ulimwengu mamboleo. Maaskofu wanasikitishwa sana na hali halisi wakati huu Kenya inapojiandaa kwa ajili ya uchaguzi mkuu, unaotarajiwa kufanyika hapo mwakani.

Maaskofu wanaipongeza Serikali kwa kutoa vifaa vya uandikishaji wa kura na wanataka itangazwe mapema tarehe rasmi ya kuanza kujiandikisha kupiga kura, ili wananchi waweze kupata muda mrefu wa kuweza kujiandikisha ili kushiriki katika uchaguzi mkuu ambao umepangwa kufanyika hapo tarehe 4 Machi 2013. Maaskofu wanataka Serikali iwahakikishie kwamba, tarehe hii haitabadilishwa kwa kisingizio chochote kile na kwamba, Serikali itajipanga vyema ili kuhakikisha kuwa, zoezi hili linafanyika kadiri ilivyopangwa. Ni dhamana na jukumu la wananchi wa Kenya kupiga kura, hivyo kila mwananchi anapaswa kutekeleza wajibu wake wa Kikatiba.

Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linasema kwamba, juhudi za kutaka kuwakomboa Wakenya kwa mara ya pili zinaelekea kugonga mwamba, ikiwa kama vipengele vya Katiba kuhusu uongozi havitazingatiwa na kutekelezwa ipasavyo. Uadilifu katika uongozi ni zaidi ya kuwa mwema, bali ni jambo linalodai zaidi uadilifu na tabia njema kwa wale wote wanaotafuta nafasi za uongozi nchini Kenya.

Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linapenda kuchukua fursa hii kuwaomba wananchi wote kuwapima kikamilifu wale wote wanaowania nafasi za uongozi kuhusu uadilifu wao na kwamba, wote watakaobainika kuwa na kasoro zifuatazo hawana sifa ya kuchaguliwa kuwaongoza wananchi wa Kenya. Kamwe wananchi wasiwachague viongozi ambao si wachamungu; wasiofuata sheria na wote wanaochochea raia kuvunja sheria za nchi.

Watu ambao wamekwishawahi kushitakiwa na kukutwa na makosa ya jinai, rushwa, ufisadi na kutokuwa waaminifu, hawafai kuchaguliwa. Wengine kwenye kundi hili ni wale ambao wanapandikiza mbegu ya chuki na uhasama kwa maneno au matendo yao. Wale wote wanaojihusisha kwa namna moja au nyingine na biashara haramu ya dawa za kulevya, au biashara haramu na magendo hawafai kuchaguliwa.

Watu ambao wanawatumia wengine au wanawalipa wengine ili kufanya vurugu ni sumu ya uongozi wan chi. Wananchi wasiwachague watu ambao wamekuwa ni kigeugeu katika misimamo yao kuhusiana na masuala yenye mustakabali wa taifa.

Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linasikitishwa na hali ya ukosefu wa ulinzi na usalama pamoja na ongezeko la vitendo vya kigaidi, ambao walengwa wakuu wamekuwa ni Wakristo wanapokuwa kwenye maeneo yao ya Ibada. Jambo la kusikitisha ni kuona kwamba, pale ambapo Jeshi la Polisi linaahidi kuwasaka kwa udi na uvumba wahusika wa vitendo hivi vya kigaidi ndivyo vinavyozidi kuongezeka. Maaskofu wanajiuliza, Je, watu wao wataendelea kuteseka hadili lini? Mbona wahalifu hawa hawajafikishwa kwenye mkondo wa sheria? Maaskofu wanaitaka Serikali kuhakikisha kwamba, kila mwananchi wa Kenya anakuwa na uhakika wa usalama wake.

Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linasikitika kusema kuwa, uingizaji wa silaha nchini humo unatisha. Wanawapongeza Askari wote ambao wamesimama kidete kutekeleza wajibu wao kiasi hata cha kupoteza maisha yao kwa ajili ya kulinda usalama wa raia, wanawaombea. Lakini, inasikitisha kuona kwamba, kuna baadhi ya Askari ambao wanashindwa kutekeleza wajibu wao barabara kiasi cha kuifanya biashara haramu ya silaha nchini Kenya kuendelea kushamiri kwa kasi ya ajabu, hali inayopelekea ongezeko la vitendo vya kigaidi. Wanaitaka Mahakama nchini Kenya, kutekeleza wajibu wake kikamilifu bila kuingiliwa na wanasiasa, hasa wakati huu, Kenya inapojiandaa kwa ajili ya uchaguzi mkuu.

Maaskofu wana hofu na jinsi ambavyo Serikali inaendelea kuyashughulikiapole pole masilahi ya Jeshi la Polisi. Wanajiuliza, Je, kila mfanyakazi anapaswa kugoma ili aweze kupata haki yake? Kwa sasa kuna wimbi kubwa la wafanyakazi kutaka kuboreshewa hali zao pamoja na kuongezewa mishahara jambo ambalo ni haki kabisa kabisa. Lakini Maaskofu wanasema kuwa, kitendo cha Serikali kutoa mishahara na marupurupu manono kwa baadhi ya wafanyakazi kwa kuzingatia sera baguzi ni jambo la hatari. Hali hii itapelekea mfumuko wa bei na huduma hali ambayo itakuwa na athari kubwa kwa Mkenya wa kawaida.

Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linasema kwamba, kwa siku za hivi karibuni kumekuwepo na ongezeko kubwa la wanasiasa kutaka kushirikiana na kujijenga kisiasa; dalili za ukomavu wa kisiasa, lakini kwa bahati mbaya muungano huu unafanyika kwa misingi ya Ukabila na wala si kwa ajili ya maboresho ya maisha ya wananchi wa Kenya katika ujumla wao. Maaskofu wanawaalika wanasiasa nchini humo kuhakaikisha kwamba, wanajenga na kudumisha Umoja wa Kitaifa.

Maaskofu Katoliki Kenya wanatambua vijana na karama mbali mbali walizokirimiwa na Mwenyezi Mungu katika maisha yao ya ujana: wana sifa njema, nguvu, ndoto na matumaini makubwa sit u kwa ajili yao kama alivyowahi kuonya Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, bali sifa na karama hizi zinapaswa kuwa ni kwa ajili yaw engine, Kanisa na Ulimwengu katika ujumla wake. Wanawaonya vijana kuwa makini zaidi na kamwe wasitafute kukidhi matamanio yao ya muda mfupi ambayo mara nyingi yanawaangamiza.

Wanapaswa kuona makosa yanayotendeka nchini mwao na kamwe wasikubali kutumiwa na wanasiasa wanaogubikwa na ubinafsi kwa ajili ya mafao yao bali wajikite katika kumwilisha Amri za Mungu katika maisha yao.

Mwishoni, Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya, linawaalika Waamini na Wananchi wote wa Kenya kuhakikisha kwamba, wanajitahidi kujenga mazingira yatakayosaidia kuufanya uchaguzi mkuu kuwa huru na wa haki. Ni changamoto ya kutolea ushuhuda wa imani yao wakati huu ili waweze kuwa na kipindi cha utulivu, maendeleo ya kweli, daima wakiendelea kuwa ni wachamungu.








All the contents on this site are copyrighted ©.