2012-11-10 09:07:06

Ratiba elekezi ya shughuli za Baba Mtakatifu Benedikto XVI kwa Mwezi Novemba hadi Januari 2013


Idara ya Liturujia ya Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, imetoa ratiba elekezi ya maadhimisho mbali mbali ya Kiliturjia yanayotarajiwa kufanywa na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, kuanzia tarehe 24 Novemba 2012, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican atakapowasimika rasmi Makardinali wapya walioteuliwa hivi karibuni. Na Jumapili tarehe 25 Novemba, Sherehe ya Kristo Mfalme, Baba Mtakatifu anatarajiwa kuungana na Makardinali wapya kwa ajili ya maadhimisho ya Sherehe ya Kristo Mfalme.

Tarehe Mosi Desemba, 2012, Baba Mtakatifu atakianza Kipindi cha Majilio, kwa kuadhimisha Ibada ya Masifu ya Jioni na Wanafunzi wa Taasisi za elimu na vyuo vikuu vya kipapa vilivyoko hapa mjini Roma, Ibada ambayo inatarajiwa kuanza hapo saa kumi na moja na nusu kwa saa za Italia.

Tarehe 8 Desemba, 2012, Siku kuu ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, majira ya jioni, Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, anatarajiwa kwenda kwenye Uwanja wa Spagna, ili kutoa heshima zake kwa Sanamu ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili.

Tarehe 16 Desemba, 2012, Jumapili ya tatu ya Kipindi cha Majilio, Baba Mtakatifu anatarajiwa kufanya hija ya kichungaji kwenye Parokia ya Mt. Patricia, iliyoko mjini Roma na kuongoza Ibada ya Misa Takatifu.

Tarehe 24 Desemba, 2012, Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, anatarajiwa kuongoza Ibada ya Misa Takatifu, Mkesha wa Noeli, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Ibada hii inatarajiwa kuanza saa nne kamili usiku kwa saa za Italia

Tarehe 25 Desemba 2012, Mama Kanisa atakuwa anasherehekea Siku kuu ya Noeli, kuzaliwa kwa Yesu Kristo Mwana wa Mungu. Kwa tukio hili, Baba Mtakatifu, saa sita kamili mchana kwa saa za Italia, anatarajiwa kutoa Ujumbe wa Noeli sanjari na Baraka kwa Mji wa Roma na Ulimwengu kwa ujumla kama zinavyojulikana kwa lugha ya Kilatini "Urbi et Orbi"

Tarehe 29 Desemba 2012, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, majira ya saa kumi na mbili kamili, saa za Italia, Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, anatarajiwa kuongoza Sala kwa ajili ya Vijana wa Jumuiya ya Taizè kutoka Bara la Ulaya

Tarehe 31 Desemba 2012, Baba Mtakatifu ataongoza Masifu ya Jioni na Shukrani kwa Mwenyezi Mungu " Te Deum" kwa kufunga Mwaka na kama sehemu ya Siku kuu ya Bikira Maria Mama wa Mungu.

Tarehe Mosi Januari 2013, Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, anatarajiwa kuuanza Mwaka Mpya kwa Maadhimisho ya Siku kuu ya Bikira Maria Mama wa Mungu, sanjari na Maadhimisho ya Siku ya Arobaini na sita ya Kuombea Amani Duniani.

Tarehe 6 Januari 2013 Sherehe ya Tokeo la Bwana au "Epifania", Asubuhi, Baba Mtakatifu anatarajiwa kuongoza Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Tarehe 13 Januari 2013, Jumapili baada ya Sherehe za Tokeo la Bwana, Mama Kanisa ataadhimisha Sherehe ya Ubatizo wa Bwana, kwenye Kikanisa cha Sistina sanjari na kutoa Sakramenti ya Ubatizo kwa baadhi ya watoto watakaokuwa wameandaliwa rasmi ili kuanza hija ya maisha yao ya kiroho wakisaidiwa na wazazi na wasimamizi wao wa Ubatizo.

Tarehe 25 Januari 2013, Siku kuu ya Kuongoka kwa Mtakatifu Paulo, Mtume na Mwalimu wa Mataifa, Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, anatarajiwa kuongoza Masifu ya Jioni pamoja na kufunga Juma la kuombea Umoja wa Wakristo

Ndugu msikilizaji, Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican, itakuwa nawe bega kwa bega kuhakikisha kwamba, inakujuvya kwa kina na mapana yale yote yatakayojiri katika maadhimisho haya, usikose kumshirikisha jirani yako.







All the contents on this site are copyrighted ©.