2012-11-10 11:31:38

Kanisa Anglikana lapata Kiongozi wake mkuu ni: Askofu mkuu mteule Justin Welby


Askofu Justin Welby wa Jimbo la Durham, mwenye umri wa miaka hamsini na sita, mwenye mke na watoto watano, Kanisa Anglikana atakuwa ni Askofu mkuu wa mia moja na tano wa Kanisa kuu la Cantebury na Mkuu wa Jumuiya ya Waanglikani Duniani baada ya uteuzi wake kupitishwa na Malkia wa Uingereza.

Askofu Justin Welby anachukua nafasi ya Askofu mkuu Rowan Williams ambaye anatarajiwa kung'atuka madarakani mwishoni mwa Mwezi Desemba 2012. Askofu mkuu mteule anatarajiwa kusimikwa rasimi madarakani hapo tarehe 21 Machi 2013; Ibada ambayo itafanyika kwenye Kanisa kuu la Cantebury, Uingereza. Alipewa daraja la ushemasi kunako mwaka 1992 na mwaka 2011 akawekwa wakfu kuwa Askofu.

Askofu mteule anasema, uteuzi huu ni jambo ambalo limemshtusha na kubadilisha kabisa mwelekeo wa maisha yake na kwamba, yuko tayari kuendeleza mabadiliko mbali mbali ndani ya Kanisa Anglikana, ikiwa ni pamoja na kuwaweka wanawake wakfu kuwa Maaskofu.

Kwa upande wake, Askofu mkuu Rowan Williams amempongeza Askofu mkuu mteule kwa kusema kwamba, ni mtu mwenye uzoefu na mang'amuzi makubwa katika shughuli za kichungaji, ni matumaini yake kwamba, ataweza kushirikisha karama hizi kwa ajili ya maendeleo na ustawi wa Kanisa Anglikana, lenye waamini zaidi ya millioni themanini waliotawanyika sehemu mbali mbali za dunia. Mrithi wake anachangamotishwa kuhubiri akiwa ameshikilia Biblia mkono mmoja na mkono wa pili akiwa ameshikilia gazeti, ili kumwezesha kuwa na uwiano mzuri katika maisha ya mwanadamu: kiroho na kimwili.

Ni matumaini ya Askofu mkuu Rowan Williams kwamba, Jumuiya ya Waamini wa Kanisa Anglikana, itaendelea kushikamana kama Familia Moja pamoja na kutambua dhamana na wajibu wa viongozi wa Makanisa mahalia. Kati ya changamoto kubwa anazokabiliana nazo Askofu mkuu mteule Justin Welby ni kuwaweka wanawake wakfu ili kuwa Maaskofu, jambo ambalo limesababisha mgawanyo mkubwa hatari ambayo bado ipo.

Kwa upande wake, Askofu mkuu Vincent Nichols, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza amemtumia salam na matashi mema kwa kuteuliwa kwake kuwa Askofu mkuu na kiongozi mkuu wa Kanisa Anglikana Duniani. Ni matumaini yake kwamba, ataweza kushirikisha karama na vipaji ambavyo amekirimiwa na Mwenyezi Mungu sanjari na kutoa ushuhuda wa maisha ya Kikristo nchini humo.

Ni matumaini ya Askofu mkuu Nichols kuwa, Kanisa Anglikana na Kanisa Katoliki yataendelea kushirikiana kwa karibu zaidi, kwa ajili ya kutafuta mafao ya wengi na ushuhuda wa Kanisa nchini mwao.







All the contents on this site are copyrighted ©.