2012-11-10 12:24:38

Askofu mkuu Ruwaichi ateuliwa kuwa msimamizi wa kitume, Jimbo Katoliki Shinyanga


Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, Jumamosi tarehe 10 Novemba, 2012 ameliongoza Taifa la Mungu nchini Tanzania katika mazishi ya Askofu Aloysius Balina wa Jimbo Katoliki Shinyanga; ibada ambayo imehudhuriwa na viongozi mbali mbali wa Kanisa, Dini na Serikali.

Askofu mkuu Yuda Thadeus Ruwaichi ndiye aliyeteuliwa na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, kuwa msimamizi wa kitume wa Jimbo katoliki Shiyanga. Katika mahubiri yake amekazia mambo msingi ambayo Marehemu Askofu Balina aliyakazia katika maisha na utume wake, kama njia pekee ya kumuenzi na kuendelea kumkumbuka hapa duniani.

Kwa hakika, alikuwa ni mtu wa watu, aliyefanya yote kwa ajili ya sifa na utukufu wa Mungu, kwa kumhudumia mwanadamu. Ni kiongozi aliyeonesha matumaini na furaha iliyokuwa inabubujika kutoka katika undani wa maisha yake.

Kwa upande wake, Askofu mkuu Francisco Montecillo Padilla, Balozi wa Vatican nchini Tanzania, amemwelezea Marehemu Askofu Balina kuwa ni mtu aliyejitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya ukarimu kwa jirani zake, hasa zaidi kwa wale waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii. Ni kiongozi ambaye hata katika maumivu makali na ugonjwa wake, kamwe hakulalama, bali alionesha tabasamu na tumaini.

Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania katika salam zake, amemwelezea Marehemu Askofu Balina kuwa alikuwa ni rafiki yake, ambaye walishirikiana kwa karibu sana katika masuala ya elimu na afya. Ni mtu aliyejitoa kwa ajili ya maendeleo ya watanzania wote bila ubaguzi, kumbe, kifo cha Askofu Balina ni msiba wa watanzania wote.







All the contents on this site are copyrighted ©.