Uinjilishaji wa awali na ule wa kina ni chanda na pete katika mapambazuko ya Millenia
ya Tatu ya Ukristo!
Yesu Kristo ni kiini cha Uinjilishaji Mpya unaofanyiwa kazi na Mama Kanisa katika
mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo, iwe ni katika Uinjilishaji wa awali au
Uinjilishaji Mpya, kwani anabaki kuwa ni Alfa na Omega, nyakati zote ni zake. Kanisa
kama Fumbo la Mwili wa Kristo, limepewa dhamana na utume wa kutangaza Habari Njema
ya Wokovu hadi miisho ya dunia.
Ni maneno ya Kardinali Fernando Filoni, Rais
wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu, alipokuwa anashiriki katika Kongamano
kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilee ya miaka mia moja ya Ukristo Jimbo la Owerri,
nchini Nigeria. Anasema, Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican ulitoa changamoto ya kuanzishwa
kwa Makanisa mahalia, ili yaweze kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa
na wala si kuwa ni viwanja vya shughuli za kimissionari kama ilivyozoeleka hapo awali
kabla ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican.
Ulikuwa umefika wakati kwa Kanisa
mahalia kuwa mdau mkuu wa Uinjilishaji miongoni mwa watu wake, changamoto endelevu
hata katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo. Kuinjilisha maana yake ni
kuwashirikisha na kuwamegea wengine ile furaha ya ndani ya kukutana na Yesu Kristo
mkombozi wa dunia, aliyeteswa, akafa na kufufuka, kielelezo makini cha upendo wa Mungu
kwa binadamu. Imani hii inamchangamotisha mwamini kuitolea ushuhuda katika uhalisia
wa maisha yake, daima akiendelea kutangaza matendo ya Mungu katika ulimwengu mamboleo.
Kardinali
Filoni anasema, dhana ya Uinjilishaji Mpya inapata chimbuko lake, miaka kumi baada
ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican yaani kunako mwaka 1974, Baba Mtakatifu Paulo wa
Sita alipoitisha Sinodi juu ya Uinjilishaji. Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili akaivalia
njuga dhana ya Uinjilishaji Mpya na kuipatia kipaumbele cha kwanza katika maisha na
mikakati yake ya kichungaji kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. kwa hakika, ndiye muasisi
wa neno "Uinjilishaji Mpya".
Yesu Kristo alitumwa na Baba yake wa mbinguni
kuja duniani ili kumkomboa mwanadamu, naye kwa upande wake, akawateuwa mitume miongoni
mwa wafuasi wake ili kushiriki kwa ukaribu zaidi dhamana ya kutangaza na kueneza Ufalme
wa Mungu hadi miisho ya dunia, dhamana inayotekelezwa hadi leo hii na Mama Kanisa.
Kwa hakika, Kanisa haliwezi kukaa kitako bila ya kuinjilisha kwani kwa kufanya hivi,
litakuwa linasaliti dhamana, wito na utume wake.
Linapaswa kutangaza Habari
Njema kwa umakini na ugunduzi mkubwa zaidi, ingawa dhamana hii inakabiliwa pia na
changamoto mbali mbali za maisha, ikiwa ni pamoja na madhulumu.
Kardinali Fernando
Filoni anahitimisha mchango wake kwa kuwataka waamini kuendeleza majadiliano ya kidini
na kiekumene kama njia mufaka ya Uinjilishaji Mpya katika mazingira yao, daima wakiwa
wepesi kusoma alama za nyakati, ili kuwaonjesha wengine ile furaha ya kuwa kweli ni
wafuasi wa Kristo. Kanisa bado lina changamotishwa kuendelea kuwa ni sauti ya kinabii,
inayojikita katika kutafuta mafao ya wengi, haki, amani, upendo na mshikamano wa dhati,
daima likitekeleza wajibu huu msingi kwa njia ya upatanisho wa kweli, ili dunia iweze
kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi.