2012-11-09 14:34:37

Papa akutana na kuzungumza na wajumbe wa Interpol mjini Vatican


Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, Ijumaa tarehe 9 Novemba 2012 alikutana na kuzungumza na wajumbe kutoka katika nchi mia moja na tisini wanachama wa Shirika la Interpol, waliokuwa wanahudhuria mkutano wao wa themanini na moja hapa mjini Roma, ambayo Vatican pia ni mwanachama wake tangu mwaka 2008.

Baba Mtakatifu katika hotuba yake, amekazia umuhimu wa kudumisha na kuendeleza ushirikiano wa kimataifa katika mchakato unaopania kudhibiti vitendo vya jinai duniani, kwa kushirikishana wataalam, ujuzi, uzoefu na mang'amuzi mbali mbali, kwani vitendo hivi vinadumaza maendeleo ya mwanadamu na mustakabali wa Jumuiya ya Kimataifa. Mkutano huu ni muhimu sana kwani umewakutanisha wanasiasa na wadau waliopewa dhamana ya kudumisha ulinzi, usalama na haki, kwa kuzingatia utawala wa sheria, ili kila mdau katika eneo lake aweze kutekeleza vyema wajibu huo msingi.

Viongozi wa kisiasa wanao upeo mpana wa kung'amua kwa haraka hatari zinazoweza kujitokeza katika maisha ya kijamii na hivyo kutoa mwongozo wa utekelezaji kwa vyombo husika, ili kudhibiti vitendo vya jinai. Familia ya binadamu anasema Baba Mtakatifu inaendelea kuathirika kutokana na kuongezeka kwa vitendo vya jinai, changamoto ya kulinda na kudumisha ulinzi na usalama kwa kila mwananchi na Jamii kwa ujumla, kwa kutumia nyenzo bora zinazopatikana katika mazingira husika.

Interpol inatekeleza dhamana ya ulinzi na usalama katika ngazi ya kimataifa, kwa kupania kwa namna ya pekee, kutafuta mafao ya wengi, kwa kuheshimu sheria za nchi ili watu waweze kuishi kwa amani na uelewano. Baba Mtakatifu anatambua kwamba, kuna baadhi ya wadau wa ulinzi na usalama wanafanya kazi katika mazingira hatarishi sana, hasa pale wanapowajibika kulinda maisha ya watu wengine pamoja na kuendeleza mchakato wa ujenzi wa Jamii inayosimikwa katika misingi ya amani.

Mara baada ya kumalizika kwa vita baridi, kumeibuka aina mpya ya vitendo vya jinai, mambo ambayo yanapata chimbuko lake katika masuala ya kisiasa pale ambapo vurugu na fujo ulionekana kama mtindo wa kudai uhuru wa watu ndani ya jamii dhidi ya mfumo kandamizi. Kinzani za kivita zinaendelea kupungua lakini vitendo vya jinai vinaongezeka siku hadi siku kiasi cha kuhatarisha usalama na maisha ya watu wengi zaidi duniani, bila kusahau changamoto kwa wakuu wa nchi husika.

Kanisa litaendelea kuunga mkono wote wanaosimama kidete kupinga na kudhibiti vitendo vya jinai ambavyo kwa sasa vinaanza kuchukua sura ya kimataifa, kama vile vitendo vya kigaidi, vinavyopandikiza mbegu ya chuki, uhasama, kifo na tabia ya kutaka kulipizana kisasi. Ni vitendo vinavyosababisha uharibifu mkubwa wa mali na maisha, vinagumisha mtandao wa kisiasa kutokana na matumizi ya teknolojia ya hali ya juu kabisa na kiasi kikubwa cha fedha haramu ili kugharimia vitendo hivi.

Matokeo yake ni kumwingiza mwanadamu katika utumwa mamboleo, biashara haramu ya malighafi, matumizi haramu ya dawa za kulevya, silaha, magendo, dawa zisizo na viwango ambazo kwa masikitiko makubwa zinasafirishwa na kutumiwa na watu wanaoishi katika nchi zinazoendelea duniani, badala ya kutibu dawa hizi zinakuwa ni chanzo cha vifo vyao. Kuna mfumuko wa biashara haramu ya viungo vya binadamu hali ambayo inadhalilisha utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Ni watu wanaokwenda kinyume na misingi ya maadili na utu wema.

Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, anabainisha kwamba, vitendo vya jinai, vinaendelea kuacha madonda makubwa katika utu na heshima ya binadamu, changamoto kwa wadau mbali mbali kusimama kidete kudhibiti vitendo vyote hivi, kwa kuzingatia maadili ya kazi, utawala wa sheria na haki msingi za binadamu. Mkakati huu si suala la Jeshi la Polisi peke yake, bali ni dhamana ya kila mtu ndani ya jamii kujenga na kuimarisha misingi ya haki na amani ili kuondokana na mbegu ya chuki, uhasama na hali ya kupenda kulipizana kisasi.

Changamoto hii inapaswa kufanyiwa kazi anasema Baba Mtakatifu na Jamii nzima, lakini zaidi katika: Familia, taasisi za elimu na vyuo vikuu, dini, vyombo vya mawasiliano ya jamii na kwamba, kila mwanachi ana dhamana ya kujenga misingi ya haki na amani. Baba Mtakatifu amehitimisha hotuba yake kwa kuwashukuru viongozi wa Interpol kwa ushirikiano mkubwa wanaoutoa kwa vikosi vya ulinzi na usalama vya Vatican, hasa zaidi wakati wa hija zake za kichungaji, sehemu mbali mbali za dunia.







All the contents on this site are copyrighted ©.