Marehemu Askofu Balina mtu wa watu na chachu ya maendeleo apumzike kwa amani!
Monsinyo Pius Rutechura, Makamu mkuu wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki Afrika Mashariki
na Kati, CUEA anasema wameupokea msiba wa Askofu Aloysius Balina wa Jimbo Katoliki
Shinyanga anayezikwa Jumamosi tarehe 10 Novemba 2012 kwa mshtuko, imani na matumaini
katika maisha ya uzima wa milele.
Binafsi alimfamu
Askofu Balina kwa karibu zaidi alipokuwa Katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki
Tanzania na baadaye alipokuwa Katibu mkuu wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki
Afrika Mashariki na Kati, AMECEA. Kwa hakika, alikuwa ni mtu wa watu, mchangamfu na
aliyewajali wote bila ubaguzi. Alikuwa na kipaji cha ugunduzi na daima aliibuka na
mawzo na changamoto mpya zilizopania kumletea mtanzania maendeleo endelevu: kiroho
na kimwili.
Alitamani kuona kwamba, Kanisa linakuwa mstari wa mbele katika
huduma kwa kuzingatia misingi, maadili na Mapokeo ya Kanisa, ili liweze kujitegemea
kwa raslimali watu walioandaliwa barabara, tayari kuchakarika kwa ajili ya maendeleo
ya nchi yao. Matunda yanaonekana katika Sekta ya Afya.