2012-11-09 08:33:27

Maadhimisho ya Mwaka wa Imani; umuhimu na changamoto zake!


Askofu Michael Msonganzila wa Jimbo Katoliki Musoma anasema, Mwaka wa Imani uliotangazwa na kuzinduliwa na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, ni mwaliko wa kutambua kwa mara nyingine tena kwamba, imani ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayopaswa kumwilishwa katika fadhila ya upendo kwa Mungu na jirani. RealAudioMP3

Maadhimisho ya Mwaka wa Imani yanakwenda sanjari na Jubilee ya miaka 50 ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, wenye utajiri mkubwa, ambao ukitumika kikamilifu basi waamini wataweza kuinesha imani yao katika maadhimisho mbali mbali ya Liturujia ya Kanisa, kupenda kusoma na kulitafakari Neno la Mungu ambayo ni taa na dira ya maisha ya mwamini; watawajibika kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa na zaidi ya hayo, watajitakatifuza ili waweze kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda makini wa imani yao kwa Kristo na Kanisa lake.

Matunda ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican ni Sheria Mpya za Kanisa zilizotolewa kunako mwaka 1983; Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki; muhtasari wa Imani, Sakramenti za Kanisa, Maisha adili na Maisha ya Sala. Ni Katekisimu inayodai maandalizi makini na ya kina ili kufahamu kweli za Kikristo ambazo zinapata chimbuko lake katika Biblia, Mapokeo ya Kanisa na Mafundisho ya Mababa wa Kanisa.

Mwaka wa Imani unawachangamotisha waamini kutolea ushuhuda wao kwa Kristo aliyeteswa, akafa, akafufuka kutoka katika wafu, akapaa mbinguni, atarudi tena kuwahukumu wazima na wafu na wala ufalme wake hautakuwa na mwisho. Ni mwaliko wa kukema maovu, kudumisha majadiliano ya kidini na kiekumene, ili kukabiliana na kinzani na migogoro ya kidini, ukanimungu ili hatimaye, kujenga utamaduni wa kuheshimiana na kuvumiliana hata katika tofauti za kiimani ambazo zinapaswa kuwa ni utajiri kwa kila mtu.

Ni jukumu la viongozi mbali mbali kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kukemea, kuonya na kudhibiti chokochoko za kidini, kwani zinaweza kuleta maafa makubwa katika Jamii. Mwaka wa imani uwajengee waamini uwezo wa kukemea maovu jamii kama vile: rushwa, ufisadi, mila na tamaduni potofu, kwa njia ya ushuhuda makini unaoleta mvuto na mguso katika maisha ya jamii.

Mwaka wa Imani uwatie waamini ari na shauku ya kuieneza, linda na kuitetea imani yao hadi dakika ya mwisho ya maisha yao. Wawe ni mfano wa kuigwa katika kujenga na kutetea amani, haki, upendo na mshikamano wa kweli.







All the contents on this site are copyrighted ©.