2012-11-08 08:47:37

Vijana katika pilika pilika za maisha, mpokeeni Yesu ili aweze kuwa kweli ni mwenza wenu katika hija ya maisha ya ujana!


Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu ambaye yuko nchini Nigeria kushiriki katika Maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 100 ya Ukristo Jimboni Owerri, katika mkutano wake wa kwanza na vijana pamoja na watoto wa Jimbo Katoliki la Owerri, Jumanne, tarehe 7 Novemba 2012, amewataka kumpokea kristo kwa moyo wa unyenyekevu, ili aweze kuwa ni mwenza katika hija ya maisha yao ya ujana, wanapokuwa: nyumbani, shuleni, maeneo ya kazi na njiani.

Hii ni kutokana na ukweli kwamba, vijana ni tumaini na jeuri ya Kanisa na kwamba, wao ni matunda ya juhudi za Uinjilishaji, uliofanywa na Wamissionari takribani miaka mia moja iliyopita. Kardinali Filoni ameyasema hayo wakati wa maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya vijana na watoto wa Jimbo Katoliki la Owerri, Nigeria.

Vijana kwa namna ya pekee, wanaalikwa kutafakari kwa kina Neno la Mungu ili liweze kuwa ni taa na dira katika hija ya maisha yao hapa duniani. Matukio na vitu vyenye mvuto kutoka katika kazi ya uumbaji, ni kati ya njia ambazo Yesu Kristo anazitumia kuzungumza na waja wake. Wanapaswa kutambua kwamba, kila dakika ya maisha yao, wanapaswa kumtumainia Mwenyezi Mungu na kwamba, bila Mungu, maisha yao yatakuwa makavu kama kigae!

Kardinali Filoni anawataka vijana kujenga na kudumisha utamaduni wa kupenda kujifunza kusali kwa Ibada na uchaji wa Mungu. Watolee sala kwa ajili ya mahitaji yao binafasi, wakikumbuka kusali pia kwa ajili ya jirani zao, ili hatimaye, waweze kuwa kweli ni sadaka safi kwa wale wanaowazunguka.

Huu ni mwaliko wa kumwendea Yesu, wanapoelemewa na mizigo ya maisha, wanapochoka na kukata tamaa kutokana na pilika pilika za maisha ya ujana, kwani Yeye atawapumzisha. Ni jukumu la vijana kutafuta fursa ya kukaa pamoja na Yesu kwa njia ya ukimya na tafakari ya kina, kwani kwa hakika, hatawaangusha wala kuwatelekeza!







All the contents on this site are copyrighted ©.