Salam na matashi mema kwa Rais Barack Obama kutoka kwa Baraza la Maaskofu Katoliki
Marekani
Baraza la Maaskofu Katoliki litaendelea kusimama kidete kulinda na kutetea Injili
ya Maisha, tunu msingi za maisha ya ndoa na familia pamoja na uhuru wa kidini. Maaskofu
wanamwomba Rais Barack Obama wa Marekani kuendelea kujitoa kwa ajili ya wote wanaosukumizwa
pembezoni mwa Jamii, hususan watoto ambao bado hawajazaliwa, maskini, wageni na wahamiaji
pamoja na kuhakikisha kwamba, anakabiliana kwa nguvu, hekima, nidhamu na utashi mkubwa
changamoto zilizoko mbele ya wananchi wa Marekani.
Ni maneno ya Kardinali Timothy
Dolan, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani, katika ujumbe wake wa pongezi
na matashi mema kwa Rais Barack Obama kwa kuchaguliwa kwake kuwaongoza Marekani kwa
kipindi kingine cha miaka minne.
Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani linamwombea
Rais Obama ili aweze kutekeleza wajibu wake kwa kutafuta kwanza kabisa mafao ya wengi
na kwamba, mijadala inayofanyika nchini humo, itazingatia heshima na upendo kwa kila
mmoja, badala ya matumizi mabaya ya majukwaa kama ilivyojitokeza kwa siku za hizi
karibuni. Mwishoni, wanamtakia kila la kheri na baraka tele Rais Obama na Makamu wake
Biden, wakati huu wanapoanza kuwaongoza Wamarekani kwa awamu ya pili.