2012-11-08 07:58:56

"Endeleeni kumuenzi Marehemu Askofu Balina kwa njia ya huduma makini kwa binadamu; kwa kudumisha, umoja, upendo na mshikamano wa dhati"


Askofu Michael Msonganzila wa Jimbo Katoliki la Musoma, Tanzania anasema, wakati huu ambapo Familia ya Mungu nchini Tanzania inaendelea kuomboleza kifo cha Askofu Aloysius Balina wa Jimbo Katoliki Shinyanga, ikumbukwe kwamba, Mwenyezi Mungu amemuumba mwanadamu kwa sura na mfano wake, anataka binadamu amfahamu, ampende na kumtumikia. Amempatia mwanadamu Amri kuu ya Upendo kwa Mungu na jirani. RealAudioMP3

Yote haya yamejidhihirisha katika maisha na utume wa Marehemu Askofu Balina wa Jimbo Katoliki Shinyanga, wakati alipokuwa anatekeleza dhamana na wajibu wake wa kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Ni mwaliko wa kuendelea kumuenzi Askofu Balina kwa kudumisha umoja, upendo na mshikamano wa dhati, bila kusahau kuwahudumia jirani kwa moyo, akili na nguvu zote, kama sehemu ya kushiriki katika kazi ya ukombozi iliyoanzishwa na Kristo mwenyewe.

Mshtuko wa kifo cha Askofu Balina, kamwe kisiwe ni chanzo cha utengano, bali Taifa la Mungu liendelee kuupokea msiba huu kwa imani, matumaini na mapendo, daima wakijitahidi kuyatafakari mapenzi ya Mungu katika maisha yao. Ni mwaliko wa kuendelea kumwombea pamoja na kuanza kuliombea Jimbo Katoliki la Shinyanga, ili liweze kuwa tayari kumpokea Askofu mwingine, atakayeteuliwa na Mama Kanisa kuiongoza Familia ya Mungu Jimboni humo.

Matukio yote haya yanayofumbatwa katika maadhimisho ya Mwaka wa Imani, yawasaidie waamini kuyapokea pia kwa imani na kwa kutambua kwamba, kwa hakika Mwenyezi Mungu bado anaendelea kuwasikiliza na atazijibu sala zao kwa wakati muafaka.







All the contents on this site are copyrighted ©.