Vitendo vya jinai vimeongezeka maradufu duniani kutokana na utandawazi, maendeleo
ya sayansi na teknolojia pamoja na matumizi ya fedha haramu
Askofu mkuu Dominique Mamberti, Katibu mkuu wa mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa
mjini Vatican, ni kati ya viongozi waliotoa mada wakati wa maadhimisho ya mkutano
wa themanini na moja wa Shirika la Interpol, unaotarajiwa kufungwa rasmi Alhamisi
tarehe 8 Novemba, 2012.
Wajumbe wa mkutano huu wanapembua kwa kina na mapana
changamoto ambazo Jeshi la Polisi linakumbana nazo katika mapambano dhidi ya vitendo
vya jinai sehemu mbali mbali za dunia. Katika kipindi cha miaka kumi iliyopita, vitendo
vya jinai vimeongezeka maradufu katika mifumo mbali mbali kiasi cha kuhatarisha ulinzi
na usalama wa raia na mali zao.
Ni matukio ambayo wakati mwingine yanavuka
mipaka ya nchi kutokana na utandawazi, maendeleo ya sayansi na teknolojia pamoja na
matumizi ya fedha haramu. Mikakati ya ulinzi na usalama haina budi kutoa kipaumbele
cha kwanza kwa binadamu, utu na heshima yake bila kusahau haki zake msingi kama zilivyobainishwa
kwenye Azimio la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa. Ni changamoto kwa Jeshi la
Polisi kuhakikisha kwamba, linatafuta sababu za vitendo hivi vya jinai ili hatimaye,
kuvikomesha.
Serikali kwa upande wake, hazina budi anasema Askofu mkuu Mamberti
kukuza na kuimarisha utawala wa sheria; Bunge na Mahakama zitekeleze nyajibu zao bila
kuingiliwa kwa kuzingatia misingi ya: uwajibikaji, ukweli na uwazi na kwamba, sheria
ni sawa kwa wote na hakuna mtu ambaye yuko juu ya sheria.
Jumuiya ya Kimataifa
inachangamotishwa kuhakikisha kwamba, inaweka mazingira yatakayodumisha utawala wa
sheria, kwa ajili ya kutafuta mafao ya wengi bila kusahau mambo msingi yanayopelekea
kushamiri kwa ukosefu wa haki ndani ya Jamii husika. Ni vyema zaidi Jamii ikajitahidi
kuzuia vitendo vya jinai, kwa kushirikiana na wananchi wenyewe kwani ulinzi na usalama
wa raia na mali zao, uko pia mikononi mwao wenyewe.
Jamii isimamie kidete
kulinda na kutetea tunu msingi pamoja na kuendelea kutoa malezi bora kwa watoto kuhusu
utii wa sheria na mamlaka husika kuanzia ndani ya familia, ambayo kimsingi inapaswa
kuwa ni chemchemi ya upendo. Wazazi na walezi anasema Askofu mkuu Dominique Mamberti
ni walezi wa kwanza wanaowaonjesha watoto wao haki na msamaha, tunu ambazo ni muhimu
sana katika kukuza na kudumisha uhusiano mwema ndani ya Jamii husika.