Toleeni ushuhuda wa umoja katika imani, ili kweli muweze kuwa ni wadau wakuu wa Uinjilishaji
Mpya!
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, ameendelea kusoma alama za nyakati ili kuleta
umoja, amani na mshikamano ndani ya Kanisa kwa kutambua kwamba, Liturujia ya Kanisa
ni tendo la kumtukuza Mwenyezi Mungu na mwanadamu kutakatifuzwa.
Baba Mtakatifu
kunako mwaka 2007 alichapisha Waraka wa Kichungaji uliopembua namna mbali mbali za
maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa, kabla ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican na mabadiliko
haya yakaanza kutumika tarehe 14 Septemba 2007. Katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba
yake na Kardinali Tarcisio Bertone, Katibu mkuu wa Vatican, kwenda kwa Wanachama wa
Chama cha Mahujaji Kimataifa, Baba Mtakatifu anaendelea kuhimiza umuhimu wa kuendelea
kuhifadhi utajiri unaobubujika katika maisha ya imani na sala ya Kanisa kwa kuthamini
utajiri wa tunu na maadhimisho mbali mbali ya Liturujia ya Kanisa Katoliki.
Baba
Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, anasema, Jubilee ya Miaka 50 ya Mtaguso mkuu
wa Pili wa Vatican unaokwenda sanjari na maadhimisho ya Mwaka wa Imani, ni mwaliko
kwa waamini kutolea kwa namna ya pekee, ushuhuda wa umoja katika imani na kwa njia
hii, wataweza kuwa kweli ni wadau wakuu wa Uinjilishaji Mpya, utume unaofanyiwa kazi
na Mama Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo.
Chama cha
Mahujaji Kimataifa kutoka Ufaransa, kilihitimisha hija yao mjini Roma kwa maadhimisho
ya Ibada ya Misa Takatifu, iliyoongozwa na Kardinali Antonio Canizares, Mwenyekiti
wa Baraza la Kipapa la Ibada na Nidhamu ya Sakramenti za Kanisa. Waamini hao walitumia
Misale ya Misa Takatifu iliyokuwa inatumika mwaka 1962, iliyokuwa imeidhinishwa na
Baba Mtakatifu Yohane wa ishirini na tatu kabla ya kufutwa na mabadiliko yaliyoletwa
na Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican.