2012-11-07 14:38:11

Mwaka wa Imani, iwe ni hija binafsi ya kukutana na Mwenyezi Mungu


Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, katika Maadhimisho wa Mwaka wa Imani, Jumatano tarehe 7 Novemba 2012 wakati wa Katekesi yake, aligusia kwa namna ya pekee, kiu ya kumwona Mwenyezi Mungu ambayo iko katika undani wa moyo wa mwandamu.

Mwenyezi Mungu amemuumba mwanadamu kwa ajili yake kama anavyobainisha Mtakatifu Augustino, Askofu na Mwalimu wa Kanisa na kwamba, moyo wa mwanadamu kamwe hauwezi kutulia hadi pale utakapotulia mbele ya Mwenyezi Mungu. Hata leo hii katika ulimwengu mamboleo, kiu hii bado inajionesha anasema Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita. Hii ni kiu ambayo inataka kujionesha kwa njia ya upendo.

Katika fadhila ya upendo, mwanadamu anatafuta mema kwa ajili ya jirani yake; ni changamoto na mwaliko wa kujitoa kama sehemu ya mchakato unaopania kusafisha na kuponya roho zao.

Katika hali ya urafiki na mang'amuzi ya uzuri sanjari na kiu ya kutaka kufahamu ukweli na wema, mwanadamu anahisi kwamba, ameshikwa katika mchakato ambao uko nje ya maisha yake mwenyewe; fumbo ambalo linamhakikishia mwanadamu utimilifu wa maisha yake. Mwelekeo huu wa kidini unawasaidia waamini kuweza kufungua mioyo yao ili kupokea zawadi ya imani, inayomfanya mwamini kujisikia kuwa karibu zaidi na Mwenyezi Mungu, chemchemi ya mema yote na anayekata kiu ya matamanio ya ndani kabisa ya binadamu.

Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, anawaalika waamini katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, kusali kwa ajili ya kuwaombea jirani zao wanaotafuta ukweli kwa moyo mnyofu, ili siku moja waweze kugundua na kuonja ile furaha na uhuru wa kuzaliwa katika imani.







All the contents on this site are copyrighted ©.