Marehemu Askofu Balina alisimama kidete kutangaza Injili ya maisha, umoja na mshikamano
pamoja na kulitegemeza Kanisa mahalia
Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania linaendelea kuomboleza kifo cha Askofu Aloysius
Balina wa Jimbo Katoliki Shinyanga kilichotokea hapo tarehe 6 Novemba 2012 kwenye
Hospitali ya Rufaa Bugando, Mwanza kutokana na ugonjwa wa Saratani. Mazishi yanatarajiwa
kufanyika Jumamosi, tarehe 10 Novemba 2012, Jimboni Shinyanga.
Baraza la Maaskofu
bado wanamkumbuka Marehemu Askofu Pascal Kikoti wa Jimbo la Mpanda aliyefariki dunia
hivi karibuni, lakini matokeo yote haya ni mapenzi ya Mungu.
Hayo yamesemwa
na Askofu Michael Msonganzila wa Jimbo Katoliki Musoma, wakati wa mahojiano maalum
na Radio Vatican kuhusu kifo cha Askofu Balina. Anasema, ni mtu aliyeyapokea mateso
na mahangaiko yake kwa imani kubwa, daima akimtumainia Mwenyezi mungu. Alijitoa bila
ya kujibakiza, akatumia nguvu, akili na vipaji mbali mbali alivyokirimiwa na Mwenyezi
Mungu kwa ajili ya kujenga na kuriimarisha Jimbo Katoliki la Geita, kazi ambayo ameifanya
kwa takribani miaka kumi na miwili kama Kiongozi mkuu wa Jimbo.
Kasi na mwelekeo
huo huo umejionesha pia Jimboni Shinyanga alikowatumikia waamini Jimboni humo kwa
muda wa miaka kumi na mitano, muda wa kutosha kabisa kupima mafanikio yaliyojitokeza
katika uongozi wa Askofu Balina. Kama mwenyekiti wa Idara ya Afya ya Baraza la Maaskofu
Katoliki Tanzania, alikuwa ni kiungo muhimu sana katika maboresho ya huduma ya afya
nchini Tanzania, kati ya Kanisa na Serikali chini ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.
Matunda ya mshikamano huu unaolenga mafao ya wengi yamejionesha katika huduma
bora zinazotolewa na Hospitali ya Rufaa ya Bugando na tunda lake kuu ni uanzishwaji
wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Afya na Sayansi Mwambata, CUHAS. Baraza la Maaskofu
Katoliki Tanzania, linamshukuru Marehemu Askofu Balina kwa mchango wake mkubwa katika
huduma ya afya kwa watanzania.
Askofu Balina, alisimama kidete kupinga mila
na desturi zinazokumbatia utamaduni wa kifo kwa dhana ya mauaji ya vikongwe na walemavu
wa ngozi, matukio ambayo yalichafua amani na utulivu miongoni mwa watanzania kwa ujumla.
Yote haya ni matunda ya baadhi ya watu kuendekeza na kutaka kukumbatia tamaduni na
mila potofu ambazo kimsingi zimepitwa na wakati.
Matokeo yake ni kuanzishwa
kwa Radio Faraja, ambayo kweli kimekuwa ni chombo cha Uinjilishaji wa kina unaogusa
mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Imeonesha umuhimu wa kusimama kidete kulinda,
kutunza na kuendeleza Injili ya maisha, kwa kutambua kwamba, maisha ya binadamu ni
matakatifu, kwani binadamu ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, anastahili kuheshimiwa
na kuthaminiwa.
Marehemu Askofu Balina alikazia umoja, upendo na mshikamano
wa dhati miongoni mwa wananchi wote wa Tanzania. Alijitahidi kuendeleza sera ya kulitegemeza
Kanisa mahalia kwa kutumia rasilimali iliyokuwepo kwa ajili ya utume na maisha ya
Kanisa, changamoto ambayo inapaswa kuendelea kufanyiwa kazi katika mapambazuko ya
Millenia ya tatu ya Ukristo.
Askofu Michael Msonganzila katika mahojiano haya
maalum na Radio Vatican anakiri kabisa kwamba, Marehemu Askofu Balina ameonesha unyenyekevu
wa pekee katika kuupokea ugonjwa wake na kamwe hakukata tamaa, amekuwa ni mwalimu
ambaye ameacha fundisho la kuthamini mateso katika maisha. Apumzike kwa Amani. Amina.