Kanisa Barani Afrika bado lina wajibu wa kusikiliza kwa makini sauti ya Kristo!
Mheshimiwa Dr. Thèodore C. Loko, Balozi wa Benin mjini Vatican, hivi karibuni amezindua
vitabu viwili vinavyoonesha hija ya kichungaji ya Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi
na sita nchini Benin wakati wa kuwasilisha matunda ya Awamu ya Pili ya Sinodi ya
Maaskofu wa Afrika, hapo mwaka 2011 sanjari na kumbu kumbu ya ushirikiano wa Kidiplomasia
kati ya Vatican na Benin, tukio ambalo limehudhuriwa na viongozi mbali mbali wa Kanisa
kutoka Vatican na Benin.
Hii ni kumbu
kumbu endelevu, changamoto na dhamana ya Kanisa Barani Afrika kuendelea kuisikiliza
kwa umakini mkubwa sauti ya Kristo, hasa wakati huu ambako kuna myumbo wa uchumi,
kinzani, migogoro na kumong’onyoka kwa tunu msingi za maisha adili na utu wema kutokana
na madhara ya utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Madhara haya yanajionesha
katika medani mbali mbali za maisha ya watu wengi duniani na Afrika kwa sasa wanaanza
kuonja makali yake, lakini ikumbukwe kwamba, waathirika wakubwa ni maskini na familia
zao.
Ni changamoto inayotolewa na Kardinali Robert Sarah, Rais wa Baraza la
Kipapa linaloratibu misaada ya Kanisa Katoliki, Cor Unum, alipokuwa anachangia mada
kwenye tukio hili ambalo limeacha kumbu kumbu kubwa kwa Familia ya Mungu Barani Afrika.
Anasema, dalili za myumbo wa uchumi kimataifa zilianza kujionesha kwa namna ya pekee
Nchini Marekani na Ulaya kunako mwaka 2008. Haya ni matokeo yanayopata chimbuko lake
kutokana na sera za kukumbatia utamaduni wa kifo, leo hii kuna idadi kubwa ya wazee
wanaohitaji hifadhi za kijamii, ikilinganishwa na idadi ya watoto wanaozaliwa kwenye
Familia za Nchi za Ulaya. Madhara yake yanaendelea kujionesha hata katika medani za
kijamii, kimazingira na kitamaduni.
Matokeo yake kwa Bara la Afrika anasema
Kardinali Robert Sarah ni uwapo wa wimbi kubwa la wale wanaodaiwa kuwa ni wawekezaji
Barani Afrika, wanaoendelea kukwapua maeneo makubwa ya ardhi, bila kuzingatia mafao
ya wengi na matokeo yake ni wasi wasi na woga wa mustakabali wa Bara la Afrika kwa
siku za usoni. Kuna wahamiaji wengi kutoka Asia, Uarabuni na Ulaya wanaohamia Barani
Afrika, hali ambayo imejionesha kwa namna ya pekee kwa wahamiaji kutoka Ureno kwenda
Angola na Msumbiji.
Licha ya mwelekeo huu hasi Barani Afrika, lakini pia kumekuwepo
na dalili nzuri za kukua na kuimarika kwa uchumi kwa nchi nyingi za Kiafrika, licha
ya mtikisiko wa uchumi kimataifa. Nchi nyingi Barani Afrika zina matumaini kwamba,
zinaweza kuvuka balaa la umaskini wa kukithiri miongoni mwa watu wake. Kuna dalili
za amani na utulivu kwa nchi nyingi za Kiafrika, ingawa bado migogoro ya kivita, kijamii
na kidini inaendelea kusikika kutoka sehemu mbali mbali za Bara la Afrika.
Athari
za ugonjwa wa Ukimwi; vita huko DRC, Mali, Somalia, Vitendo vya kigaidi: Nigeria,
Kenya na Tanzania ni matukio yanayoendelea kuchafua kwa kiasi kikubwa amani, utulivu
na mshikamano wa kitaifa. Kuna haja kwa Serikali mbali mbali Barani Afrika kuhakikisha
kwamba, zinalinda na kudumisha uhuru wa kuabudu, uhuru wa dhamiri, haki msingi za
binadamu na utawala wa sheria.
Kardinali Sarah anakumbusha kwamba, “Madhulumu
na Ukristo ni sawa na Mwana na Mbereko”, hali ambayo imejionesha tangu mwanzo wa Ukristo,
lakini ifahamike kuwa, damu ya mashahidi imekuwa ni mbegu ya Ukristo. Kanisa Barani
Afrika halina budi kuisikiliza sauti ya Kristo inayowaalika kutekeleza dhamana yake,
kama anavyo bainisha Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, katika Waraka wake
wa kichungaji, Africae Munus, Dhamana ya Afrika.
Hakuna maendeleo ya kweli
yasiyozingatia mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili; yasiyotambua na kuheshimu
uwapo wa Mungu wala kushughulikia mafao ya wengi na ustawi wa watu wa Bara la Afrika.
Inasikitisha kuona kwamba, kuna Mataifa Makubwa, Mashirika ya Kimataifa na Makampuni
makubwa yanayokimbilia Barani Afrika yakiwa na nguvu ya fedha, kiasi cha kutetetemesha
mawazo ya wanasiasa na hivyo kujikuta wanatelekeza dhamana na wajibu wao kwa kukumbatia
sera, mawazo na tamaduni ambazo hazina mafao wala tija kwa maendeleo na ustawi wa
Bara la Afrika.
Fedha, na ukuaji wa uchumi usiozingatia maadili na utu wema,
ni kulitumbukiza Bara la Afrika katika matatizo makubwa kwa sasa na kwa siku za usoni.
Maendeleo lazima yaguse mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Maendeleo yakuzwe
hatua kwa hatua, kwa kuwekeza katika sekta ya elimu, utu na heshima ya binadamu sanjari
na kutambua dhamana na umuhimu wa kazi, kama utimilifu wa mtu mzima.
Afya,
utunzaji bora wa mazingira, utulivu, haki, amani, umoja na mshikamano wa kitaifa;
majadiliano ya kidini, kisiasa na kiekuemene; ushiriki wa wananchi katika kupanga,
kuamua na kutekeleza masuala yanayogusa maisha yao, bila kuwasahau wanyonge na maskini.
Kuna nchi kadhaa Barani Afrika zimekuwa kweli ni mfano wa kuigwa kwa Jumuiya ya Kimataifa,
changamoto kwa nchi nyingine kujibidisha kuboresha hali ya maisha ya watu wao.
Bara
la Afrika linachangamotishwa na Mama Kanisa kusikiliza kwa makini sauti ya Kristo
na kutekeleza dhamana ya Kanisa katika Uinjilishaji Mpya, mwaliko kutoka kwa Mababa
wa Sinodi ya Maaskofu juu ya Uinjilishaji Mpya ambayo imekwenda sanjari na Maadhimisho
ya Jubilee ya miaka hamsini ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican na Mwaka wa Imani,
unaopania kwa namna ya pekee, kuwajengea uwezo waamini ili waweze kutolea ushuhuda
imani wanayoungama, adhimisha, ishi na kusali.
Wakati wa maadhimisho ya Mtaguso
Mkuu wa Pili wa Vatican, nchi nyingi za Kiafrika zilikuwa zinajipatia uhuru wake,
Kanisa likawa kweli ni mhimili mkuu wa maendeleo endelevu ya watu wa Afrika, kwa kuwapatia
matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi kwa njia ya huduma bora katika sekta ya
elimu, afya na maendeleo endelevu. Kanisa Barani Afrika, likapewa changamoto ya kuwa
ni la Kimissionari ili kujitosheleza kwa rasilimali watu katika mchakato wa Uinjilishaji
kwa ajili ya Bara la Afrika na Ulimwengu kwa ujumla wake.
Kanisa Barani Afrika
bado lina dhamana ya kuwatangazia watu Habari Njema, kwa kuendeleza dhamana ya Kanisa
kama Familia ya Mungu inayowajibika, kwa kukuza na kudumisha, umoja na mshikamano
wa Kikanisa. Kanisa halina budi kuwa karibu na watu katika hija ya maisha yao ya kila
siku: wakati wa raha na karaha, wakati wa furaha na majonzi, daima likijitahidi kutangaza
Injili ya Upendo.
Kanisa Barani Afrika linapaswa kujikita katika mchakato
utakaoliwezesha kuwa kweli ni sauti ya kinabii, inayopania kukuza na kudumisha haki,
amani na upatanisho. Amani inafumbatwa katika nguzo ya: ukweli, uhuru, haki na upendo,
kama alivyobaianaisha Baba Mtakatifu Yohane wa Ishirini na Tatu, katika Waraka wake
wa Kichungaji, Amani Duniani “Pacem in Terris”
Kardinali Robert Sarah anahitimisha
mchango wake kwa kusema kwamba, Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, ana matumaini
makubwa kwa Kanisa la Bara la Afrika, yanayofumbatwa ndani ya tunu msingi za kiutu
na maisha ya kijamii. Familia ya Mungu Barani Afrika, isikatishwe tamaa kuzionesha
na kuzimwilisha tunu hizi kama sehemu ya mchango wake kwa maendeleo na ustawi wa mwanadamu.