2012-11-07 11:16:51

Familia za Kikristo ni rasilimali nyeti katika malezi na jitihada za kurithisha imani, maadili na utu wema!


Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, Jubilee ya miaka 50 ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, Kumbu kumbu ya miaka 20 ya Katekesi Mpya ya Kanisa Katoliki pamoja na maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu juu ya Uinjilishaji Mpya ni matukio ambayo yanapania kukoleza na kuimarisha: Imani katika ushuhuda unaopaswa kujionesha katika uhalisia wa hija ya maisha yao ya kila siku.

Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, anaendelea kukumbusha kwamba, Familia za Kikristo ni rasilimali nyeti katika malezi na jitihada za kurithisha imani hii kama sehemu ya mchakato wa kujenga na kuimarisha Kanisa, ili liweze kuonesha ile sura yake ya kimissionari, kwa kujikita katika umoja, upendo na mshikamano wa dhati. Ushuhuda huu udhihirishwe katika medani mbali mbali za maisha.

Askofu Evaristo Chengula wa Jimbo Katoliki la Mbeya, hivi karibuni ameendelea kukumbushia umuhimu wa kujenga utamaduni wa kusali, kusoma na kutafakari Neno la Mungu, kushiriki kikamilifu katika Liturujia ya Kanisa sanjari na kupokea sakramenti mbali mbali za Kanisa, kama chemchemi ya neema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu, tayari kupambana na changamoto mbali mbali zinazojitokeza katika hija ya maisha yao. Ni mwaliko wa kutolea ushuhuda amini na makini wa Imani wanayoungama, wanayo isali na kuimwilisha katika matendo mema, kwa njia ya sala.

Askofu Chengula ameyasema hayo wakati wa Maadhimisho ya Sakramenti ya Kipaimara, aliyotoa kwa Waamini mia moja na kumi, katika Ibada iliyofanyika kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Anthony wa Padua, Jimbo Katoliki la Mbeya. Umefika wakati kwa wazazi na walezi kuthubutu kufanya mabadiliko katika hija ya maisha yao ya kiimani, kwa kuwajengea watoto wao hamu na kiu ya kutaka kukutana na Mwenyezi Mungu, ili aweze kuizima kiu hii kutoka katika undani wao.

Wajifunze kusali kwa bidii na uchaji, Msalaba wa Kristo uwe ni nembo ya ushindi katika magumu na changamoto za maisha, kamwe wasikate tamaa bali wasonge mbele kwa imani na matumaini. Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo, mchango mkubwa ambao unatolewa na Kanisa Barani Afrika katika mchakato wa Uinjilishaji Mpya, iwe ni shule ya Neno la Mungu, Sala na Matendo ya huruma. Chuki, hasira wala kulipizana kisasi ni mambo ambayo hayajemjengi mwamini, bali wajikite katika kutafuta na kudumisha haki, amani, upendo na mshikamano wa dhati.

Wazazi na walezi wajifunze kuwa ni walezi bora, kwa kuwakubali, kuwapokea na kuwalea watoto wao kadiri ya misingi ya Kikristo na kiutu. Wajenge na kuimarisha utamaduni wa kusikilizana, kusamehe na kusahau, tayari wakiwa na lengo la kuanza upya hija ya maisha yao hapa duniani. Amri za Mungu ziwe ni dira na mwongozo wa maisha yao hapa duniani.







All the contents on this site are copyrighted ©.