Mradi wa Maji Mwankoko, Singida kukamilika Desemba 2012
Rais Jakaya Mrisho Kikwete, Jumapili, Novemba 4, 2012, ameweka jiwe la msingi kwenye
mradi mkubwa wa maji unaolenga kumaliza tatizo la maji mjini Singida. Rais Kikwete
ameweka jiwe la msingi katika sherehe ya kufana iliyofanyika katika eneo la Mradi
la Mwankoko, nje ya mji wa Singida, mara baada ya kuwasili Mkoani Singida kuanza ziara
ya siku mbili kukagua na kuzindua miradi ya maendeleo akitokea Mkoani Manyara ambako
alifanya shughuli hizo hizo kwa siku mbili pia.
Mradi huo ulioanza kujengwa
Novemba 2, mwaka 2009, umekamilika kwa kiasi cha asilimia 80 na unatarajiwa kukamilika
ifikapo Desemba 31, 2012. Kwa mujibu wa maelezo ya wasimamizi wa Mradi wa SUWASA,
Mradi huo unagharimu dola za Marekani milioni 19.7 sawa na Sh.bilioni 31.126.
Kati
ya fedha hizo, Serikali ya Tanzania imetoa dola za Marekani milioni 10.42 sawa na
Sh. 16, 463,600,000, Benki ya Maendeleo ya Nchi za Kiarabu (BADEA) imetoa dola za
Marekani milioni 4.57 sawa na Sh. 7,220,600,000 na Mfuko wa OPEC kwa Maendeleo ya
Kimataifa wa OFID umetoa dola za Marekani milioni 4.7 sawa na Sh. 7,426,000,000.
Mradi
huo unaotekelezwa na Kampuni ya Spencon Services Limited unatarajiwa kutoa lita 17,208,000
kwa siku kutokana na visiwa viwili vilivyoko Mwankoko vyenye uwezo wa kuzalisha lita
292,000 kwa saa na visima viwili vilivyoko eneo la Irao vyenye uwezo wa kuzalisha
tani 425,000. Mradi unatarajiwa kutoa huduma kwa jumla ya wateja 3,500 kati yao 2,500
katika awamu ya kwanza na wengine 1,000 katika awamu ya pili.
Mradi utaongeza
upatikanaji wa maji kwa karibu kiasi cha asilimia 100 kwa wakazi wa mji wa Singida
na utaongeza muda wa kupatikana maji kutoka saa tano za sasa kwa siku hadi saa 24
kwa siku.