J.K. aweka jiwe la msingi la ukarabati wa barabara ya Minjingu- Arusha
Mawaziri Wakuu wa zamani pamoja na wapinzani wa CCM wamempongeza Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete na Serikali yake kwa juhudi
kubwa za kuleta maendeleo nchini na utekelezaji wake wa kiwango cha juu wa Ilani za
Chama cha Mapinduzi (CCM) za Chaguzi Kuu za 2005 na 2010.
Pongezi hizo zimetolewa
na waliokuwa Mawaziri Wakuu Waheshimiwa Frederick Tluway Sumaye na Edward Lowassa
wakati wa ziara ya Rais Kikwete katika mikoa ya Arusha na Manyara, ziara ambayo imehitimishwa
Jumatatu, Novemba 5, 2012.
Katika pongezi zake kwa Rais Kikwete, Mheshimiwa
Lowassa amesema: “Mheshimiwa Rais naomba radhi kwa kushindwa kuhudhuria shughuli ya
leo kwa sababu niko Ujerumani nikifanyiwa uchunguzi na uangalizi wa macho yangu na
afya yangu kwa jumla. Lakini Mheshimiwa Rais tunakupongeza sana na kukushukuru kwa
miradi uliotujengea katika Mkoa wa Arusha.”
Mheshimiwa Lowassa ameongeza kumwambia
Rais Kikwete katika ujumbe wa simu (sms) ambayo amemtumia Mkuu wa Wilaya ya Monduli
Mheshimiwa Njowika Kasugga na ambao aliusoma kwenye sherehe ya uwekaji jiwe la msingi
kwenye ukarabati wa Barabara ya Minjingu-Arusha juzi, Jumamosi, Novemba 3, 2012:
“Kwa
hakika umetekeleza vizuri na kwa uaminifu Ilani za Chama cha Mapinduzi (CCM) za 2005
na 2010. Tunajivunia mafanikio yako haya. Tunajivunia uongozi wako. Wewe ni kiongozi
mkuu ambaye umesimamia vizuri maendeleo ya nchi yetu na uongozi wa nchi yetu. Ndiyo
maana tutakapokutana kwenye Mkutano Mkuu wa Chama chetu wiki ijayo kila mwana-CCM
atakuwa anasimama kifua mbele.”
Naye Mheshimiwa Sumaye amemwambia Rais Kikwete:
“Sisi wana-Katesh tunakushukuru sana kwa kutufikiria na kutuweka katika ratiba yako
kwenye ziara yako hii. Aidha, Mheshimiwa Rais tuko pamoja na Serikali yako, tunakupongeza
sana kwa mafanikio mengi ambayo yamepatikana katika kipindi cha uongozi wako. Tunaipongeza
sana Serikali yako kwa kazi nzuri na tunaitambua kazi hiyo.”
Mheshimiwa Sumaye
alikuwa anazungumza kwenye mkutano wa hadhara ambao ulihutubiwa na Rais Kikwete mjini
Katesh wakati akiwa njiani kwenda Singida kwa ziara ya siku mbili kukagua na kuzindua
miradi ya maendeleo.
Akizungumza kwenye mkutano huo huo, Mbunge wa Viti Maalum
wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mheshimiwa Rose Kamili amemshukuru
Rais Kikwete na Serikali yake kwa kutimiza ahadi zake.
Mheshimiwa Kamili amemwambia
Rais Kikwete: “Tunakushukuru na kukupongeza kwa kutimiza ahadi zako na ahadi za Serikali
yako kwa wananchi wakiwamo wananchi wa Hanang.” Pongezi hizo za Mheshimiwa Kamili
zimekuja kufuatia pongezi za namna hiyo ambazo zimetolewa na Mwenyekiti wa CHADEMA,
Mheshimiwa Freeman Mbowe, Mbunge wa Rombo (CHADEMA), Mheshimiwa Joseph Selasini na
Mbunge wa Vunjo, Mheshimiwa Augustine Mrema wakati wa ziara ya Rais Kikwete katika
Mkoa wa Kilimanjaro.