2012-11-05 15:45:26

Pongezi za Papa kwa Patriaka Mpya Anba Tawadros


Baba Mtakatifu Benedikto XVI, amepeleka salaam zake za pongezi kwa Patriaki mpya wa Kanisa la Kikoptik la Kiothodox la Alexandria na upatriaki wote wa Jimbo Takatifu la Mtakatifu Marko, aliyechaguliwa Jumapili iliyopita. .
Katika salaam hizo, Papa Benedikto XV1, ameahidi kushirikiana na Kiongozi huyo mpya, aliyemwombea pia neema na baraka nyingi za Mwenyezi Mungu, ziweze kumwongoza katika kazi yake mpya atakayo ianza hivi karibuni. Na ameonyesha imani yake kwamba, atarithi mema yote yaliyoanzishwa na mtagulizi wake Papa Shenouda III, katika kuwa kiongozi wa kweli wa kiroho kwa watu wake na mshiriki aminifu, kwa raia wenzake katika kulijenga taifa jipya la Misri, kwa amani na maridhiano, na kwa ajili ya manufaa ya watu wote wa Mashariki ya kati .

Papa Benedikto ameendelea kusema, katika nyakati hizi zilizojaa changamoto, ni muhimu kwa Wakristu wote kuungana na kutolea shuhuda kwa upendo na usharika unaowaunganisha wote, kupitia utendaji, kama alivyoomba Bwana wakati wa karamu ya mwisho:ili wote waweze kuwa wamoja , ili dunia isadiki .

Na amemshukuru Mungu kwa hatua muhimu zilizopigwa , chini ya uongozi wa mtagulizi wake Papa Shenouda , katika ujenzi wa mahusiano mazuri kati ya Kanisa la Kikoptik la Kiotodosi na Kanisa Katoliki , na pia katika uaminifu wa tumaini na sala wanazoendelea kuzitolea kwa kwa ajili ya urafiki na majadiliano, yanayoongozwa na Roho Mtakatifu , kwamba, yataweza kuzaa matunda ya mshikamano wa karibu zaidi na mapatano ya kudumu.

Mungu wetu Baba Mbinguni na akujaze amani na nguvu kwa ajili ya kazi hii muhimu inayokusbiri.

Vivyo hivyo , wana siasa na maofisa wa serikali kadhaa wa Misri waonyesha kufurahia kuchaguliwa kwa Askofu Tawadros, Askofu Msaidizi wa Beheria , kuwa Patriaki mpya wa kanisa la Kikoputiki la Kiotodosi la Misri, kuchukua nafasi ya Marehemu Shenouda III.

Uchaguzi huo , ulifanyika Jumapili iliyopita, ambamo jina la Askofu Anba Tawadros, lilichukuliwa mtoto kati ya vikaratasi vya majina, vilivyokuwa pamoja kisadukuni, baada ya Ibada ya Misa katika Kanisa Kuu la kikoptiki la Mjini Cairo.

Waziri Mkuu wa Misri Hisham Kandil , pia ametoa pongezi zake kwa Wakoptic wote kupitia njia ya facebook kwa Papa Tawadros kuchaguliwa, akisema, ni heshima ya kitaifa,na historia ya Kanisa la Misri. Vivyo hivyo , viongozi wa kijeshi na maofisa wengine wametoa pia pongezi zao kwa uchaguzi huu .

Askofu Tawadros mwenye umri wa miaka 60, anakuwa ni Patriaki wa 118, na wa kwanza katika enzi ya utawala wa serikali inayoongozwa na Chama cha Kisiasa cha udugu wa kiislamu, ambacho kimeonyesha kufurahia pia kuchaguliwa kwa Tawadros.

Askofu Barnaba el Soryany , wa jijmbo la kikoptic la Kiotodosi la Mtakatifu George hapa Roma, katika mahojiano baada ya uchaguzi huo, amemtaja Papa mpya Tawadros , kuwa mtu makini katika utendaji kwa ajili ya kanisa lake na hasa Misri. Na hivyo kuchaguliwa kwake ni zawadi kubwa kwa kanisa na watu wote wenye mapenzi mema. Na hivyo wanatazamia kwamba atatembea katika mjia iliyoachwa na Marehemu Papa Shenouda III, kuwaongoza wana wake kiroho. Na hivyo wanauchukulia uchaguzi huo kuwa ni uteuzi wa Mungu.









All the contents on this site are copyrighted ©.