2012-11-05 08:33:16

Ndoa na Utawa ni miito miwili inayotegemeana ili kukamilisha upendo wa Kristo kwa Kanisa lake


Ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, nakualika tuhitimishe mfululizo wa vipindi vyetu vya ndoa na familia kwa kukiri kuwa maisha ya ndoa hayapingani na maisha ya ubikira bali uhitajiana na kwa kweli ni njia mbili tofauti za kujitoa kwa ajili ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu.
Natambua kuwa kwa nyakati mbalimbali kumekuwa na maswali mengi kuhusu upinzani au migongano kati ya maisha ya ndoa na ubikira wengi wakifanya rejea yao katika waraka wa kwanza wa mtume Paulo kwa wakorinto sura ya saba kuanzia aya ya kwanza mpaka ya thelathini na nne. (1Kor 7:1-34). Kama tulivyosema kwenye fafanuzi zetu za ndoa na familia katika maandiko matakatifu dhana hizi mbili hazipingani bali huhitajiana na kukamilishana. La msingi ni kila mmoja kuishi wito wake kwa furaha na uaminifu huku wote wakisaidiana.
Mungu aliyemuumba mwanadamu toka kwenye upendo wake anamwalika mwanadamu huyo huyo, aingie kwenye mahusiano na mwanadamu mwingine kwa kupitia mwili wake. Ni ukweli kuwa utofauti wa jinsia unadai ukamilishaji mmoja kwa mwingine. Lakini mwili huo huo, unaotumika kutajirisha upendo wa wanandoa ndio unaotumika pia kwa Watawa kujitoa kabisa sadaka kwa ajili ya ufalme wa Mungu.
Wanandoa hualikwa kujenga familia ya wanadamu ambayo pia ni familia ya Mungu. Hushirikishwa jukumu la kuleta uhai, kuulinda na kuulea. Halikadhalika wanachagua maisha ya ubikira kwa ajili ya ufalme wa Mungu hujitoa kuizaa familia ya Mungu, kuilinda na kuilea tena katika mapana zaidi.
Sasa ninaelewa zaidi kwanini baadhi ya wahudumu wa Kanisa huitwa Padre/ Father ikiwa na maana ya baba tena baba wa watoto wengi zaidi na wengine huitwa sista au mother ikiwa na maana ya mama tena mwenye watoto wengi zaidi. Nadhani ukweli huu unaendana sambamba na ahadi ya Kristo kwa wafuasi wake kuwa kuwa nyinyi mlioacha yote zikiwemo familia kwa ajili ya ufalme wa Mungu mtapata vyote zaidi zikiwemo familia mlizoacha.
Ndoa na utawa ni njia mbili za miito zinazothibisha upendo wetu kwa Kristo na Kanisa lake. Zote zinaelekeza upendo kwa mwanadamu, Zinahitajiana na zina funua upendo wa Kristo kwa Kanisa na mwili wake. Kumbe, hakuna wito ulio bora zaidi ya mwingine au dhaifu zaidi ya mwingine ila mwili wa Kristo hukamilika katika utofauti.
Kutoka Studio za Radio Vatican ni mimi Padre Raphel Mwanga, wa Jimbo Katoliki la Same, kutoka katika Taasisi ya Ndoa na Familia, Chuo Kikuu cha Kipapa Laterano- Roma.








All the contents on this site are copyrighted ©.