Waziri wa mambo ya ndani wa Italia Annamaria Cancellieri, Jumatatu, tarehe 5 Novemba
2011, amefungua mkutano wa mwaka wa themanini na moja wa Interpol unaoongozwa na kauli
mbiu "changamoto kwa Jeshi la Polisi katika kukabiliana na ghasia katika ulimwengu
mamboleo", kwa kuzitaka nchi wanachama wa Interpol, kuhakikisha kwamba, zinazidisha
na kuimarisha ushirikiano katika mapambano dhidi ya vitendo vya jinai.
Mkutano
mkuu wa Interpol unawahusisha Mawaziri wa mambo ya ndani ya nchi na Wakuu wa Jeshi
la Polisi kutoka sehemu mbali mbali za dunia, wanaojumuika kwa pamoja ili kupembua
matatizo ya usalama wanayokabiliana nayo katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo
ya sayansi na teknolojia. Mapambano dhidi ya vitendo vya jinai yanakwamishwa wakati
mwingine kutokana na mipaka na sheria za nchi, lakini wahalifu wanajikuta wakipeta
hata kuvuka mipaka ya nchi husika kwa kuendelea kila siku kutafuta mbinu ya kukwepa
mkondo wa sheria.
Kutokana na vitisho na ongezeko la vitendo vya jinai, mkutano
mkuu wa Interpol kwa mwaka 2012 umekuwa na ushiriki mkubwa kutoka kwa Mawaziri wa
mambo ya ndani ya nchi 103; nchi 169 zinawakilishwa; kuna jumla ya wawakilishi 1,100
na wakuu wa Jeshi la Polisi 81 kutoka sehemu mbali mbali za dunia.
Mada ambazo
zinafanyiwa kazi kwa sasa hadi hapo tarehe 8 Novemba 2012 ni: wahamiaji haramu; wizi
kwa njia ya mitandao; ugaidi, uharamia baharini, mapambano dhidi ya vitendo vya jinai,
biashara haramu ya nyara za taifa na fujo pamoja na ghasia mijini.