2012-11-05 09:17:12

Biashara ya silaha kimataifa haijaguswa na myumbo wa uchumi hata kidogo!


Wachunguzi wa masuala ya biashara ya silaha duniani wanabainisha kwamba, licha ya kuchechemea kwa uchumi kimataifa, lakini biashara ya silaha imeendelea kucharuka kutokana na sera za serikali nyingi kutoa kipaumbele cha kwanza katika masuala ya ulinzi na usalama lakini kwa kuzingatia kwamba, biashara ya silaha bado ina soko kubwa duniani, ndiyo maana kinzani, vita na migogoro haiwezi kuisha kamwe.

Viwanda vingi vya kutengeneza na kuuza silaha ni vile vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Serikali husika. Takwimu zinaonesha kwamba, Serikali ya Marekani inatumia kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya kununulia silaha. China, Brazil, India, Russia, Uingereza, Ufaransa, Ujerumani na Italia ni kati ya nchi ambazo zimeendelea kutumia kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya kununulia silaha.

Nchi zinazoongoza kwa utengenezaji wa silaha duniani kwa sasa ni Marekani, Uingereza, Ufaransa, Ujerumani, Italia na Russia. Silaha hizi zinapata soko kubwa katika maeneo yenye vita na kinzani za kisiasa na kijamii, kama inavyojionesha kwa wakati huu huko Mashariki ya Kati na baadhi ya nchi za Kiafrika.

Ikumbukwe kwamba, pale ambapo kunafuka moshi wa kinzani za kivita, silaha zinazotumika ni zile zilizotengenezwa katika mataifa haya: mwaka 2011, India ilikuwa ni nchi ya kwanza duniani kwa ununuzi wa silaha. Hata zile nchi ambazo uchumi wake unasua sua, lakini bado zinaendelea kutumia kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya kununulia silaha. Nchi ya Ugiriki inatumia kiasi cha asilimia nne ya Pato Ghafi la Taifa kwa ajili ua kununulia silaha. Matokeo yake ni huduma katika sekta ya elimu, afya na maendeleo ya jamii kutengewa kiasi kidogo sana cha bajeti.







All the contents on this site are copyrighted ©.