2012-11-05 08:51:24

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kuzindua Mwaka wa Imani kwenye Kanisa kuu la Mt. Yosefu, Jimbo kuu la Dar es Salaam, 9 Novemba 2012


Mwaka wa Imani ulifunguliwa rasmi na Baba Mtakatifu Benedikto wa XVI mnamo tarehe 11/10/2012. Katika kuufungua rasmi Mwaka wa Imani, Papa Benedikto aliadhimisha Ibada ya Misa maalum katika Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, mjini Vatican. Kila kanisa mahalia litapaswa pia kuadhimisha ibada maalum kwa ajili ya kufungua na kufunga Mwaka huo. Mwaka huu wa Imani utafikia kilele chake tarehe 24 Novemba 2013 katika Sherehe ya Kristo Mfalme.

Mwaka wa Imani unakwenda sanjari na maadhimisho ya Jubilee ya Miaka hamsini ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, kumbu kumbu ya miaka ishirini, tangu Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili alipochapisha Katekisimu ya Kanisa Katoliki pamoja na maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu Uinjilishaji Mpya kama nyenzo ya kueneza Imani ya Kikristo.

Hapa Tanzania, Baraza la Maaskofu Tanzania limepanga kufungua rasmi kitaifa Mwaka wa Imani tarehe 9/11/2012 kwa Ibada ya Misa Takatifu itakayoadhimishwa katika Kanisa kuu la Mtakatifu Yosefu, Jimbo kuu la Dar – es – Salaam saa 10.30 jioni. Ibada hiyo inatarajiwa kuhudhuriwa na baadhi Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania.

Baada ya ufunguzi huu wa Kitaifa, kila Jimbo litapanga ratiba ya kufungua Mwaka wa Imani Kijimbo na kupanga mikakati mbali mbali katika kuuadhimisha Mwaka huu wa Imani.

Mambo muhimu ya kufanya katika Mwaka huu wa Imani: Ni pamoja na kutafakari mwito unaoandamana na Barua ya Kitume ya Baba Mtakatifu katika Mwaka wa Imani iitwayo: Mlango wa Imani. Maneno haya Mlango wa Imani yamechukuliwa katika Biblia Takatifu Kitabu cha Matendo ya Mitume sura 14 aya 27 kwamba, Mlango wa Imani umefunguliwa kwa Mataifa yote.

Kauli mbiu ya kuadhimisha Mwaka wa Imani ni “Uinjilishaji Mpya kwa ajili ya Kueneza Imani ya Kikristo”. Hivi tunaalikwa kuangalia katika nyanja mbali mbali ni mbinu zipi zitasaidia katika Uinjilishaji mpya katika kueneza Imani ya Kikristo. Tukianza na Familia, Jumuia Ndogo Ndogo za Kikristo, Jumuia za Malezi, Vigango, Parokia na Vyama vya Kitume.

Umetolewa wimbo maalumu wenye maneno: Ninasadiki, Bwana, utuongezee Imani. Wimbo huu ni maombi ya kiulimwengu ya binadamu wote na mataifa yote, watu wa kila aina na hali, watu wa nyakati zote; ni maombi ya wanadamu kwa Muumba wao, ili Mwanga wake uwaelekee wanapoungana na Bwana Yesu Kristo, Mama Bikira Maria pamoja na watakatifu wote katika wajibu wa binadamu wote kwa Muumba wao wa kujitakatifuza na kuyatakatifuza malimwengu.

Siri kubwa ya mafanikio yao katika kuelekea Mbingu Mpya na Dunia Mpya ni kumwomba Roho Mtakatifu atawale pote wakijiaminisha katika Msalaba wa Yesu Kristo Mfufuka ili kuyamaliza matatizo yaletwayo na usiku wa maovu ya dunia hii na kuamkia upya wa uzima wa ki-Mungu.

Ni mwaliko pia kwa wataalamu wetu wa muziki wa Kanisa kuyatumia maneno ya wimbo huu na kutunga nyimbo katika mahadhi yetu hapa Tanzania zitakazotusaidia kuuishi Mwaka wa Imani kwa ushiriki hai.

Heri ya Mwaka wa Imani


Na Padre Paterni Patrick Mangi
Katibu Mtendaji, Idara ya Liturujia
Baraza la Maaskofu, Tanzania.








All the contents on this site are copyrighted ©.