Pax Christi yamtunukia Tuzo la Amani Kardinali mteule John Onaiyekan kwa kusimama
kidete kulinda na kudumisha majadiliano ya kidini
Kardinali mteule John Onaiyekan, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Abuja, Nigeria, hivi
karibuni amekabidhiwa Tuzo la Amani kutoka kwa Shirika la Amani Kimataifa, Pax Christi,
kutokana na mchango wake mkubwa katika kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini na
waamini wa dini mbali mbali Barani Afrika, lakini kwa namna ya pekee, na waamini wa
dini ya Kiislam, ili kudumisha misingi ya haki, amani, utulivu na maendeleo endelevu,
yanayogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.
Tukio hili ambalo limefanyika
kwenye Makao Makuu ya Pax Christi, limehudhuriwa na viongozi mbali mbali wa Kanisa
na Serikali na Jumuiya ya Kimataifa. Viongozi wote hawa wametambua mchango wa Kardinali
mteule Onaiyekan katika kukuza majadiliano ya kidini na waamini wa dini ya Kiislam
nchini Nigeria, mahali ambapo kwa sasa umegeuka kuwa ni "Uwanja wa Fujo" kutokana
na vitendo vya kigaidi, vinavyoendelea kuhatarisha amani, utulivu, umoja na mstakabali
wa wananchi wa Nigeria katika ujumla wao.
Kardinali mteule Onaiyekan, licha
ya vurugu zote hizi, bado hajakata tamaa na daima ameendelea kusimama kidete: kulinda,
kutetea na kudumisha misingi ya haki, amani, majadiliano ya kidini; fadhila ambazo
zimemwezesha kutunukiwa Tuzo ya Amani na Pax Christi kwa Mwaka 2012. Tuzo ya Amani
hutolewa kwa watu ambao wameonesha jitihada za pekee kabisa katika kukuza na kudumisha
haki, amani, majadiliano badala ya kuendekeza vurugu na uvunjifu wa amani kutoka sehemu
mbali mbali za dunia.
Kardinali mteule Onaiyekan anayetarajiwa kusimikwa rasmi
hapo tarehe 24 Novemba, 2012 hapa mjini Vatican, amewashukuru viongozi wa Pax Christi,
kwa kumpatia heshima kubwa kwa kuitaka Jumuiya ya Kimataifa kuchochea umoja na mshikamano;
upendo na amani, kwa kutambua kwamba, leo hii ulimwengu umekuwa kama Kijiji; kila
mtu anaguswa na yale yanayotokea hata mbali kabisa ya nchi yake.