Maadhimisho ya Mwaka wa Imani ni changamoto ya: Kusikiliza na kutekeleza utume wa
Kanisa katika mchakato wa Uinjilishaji Mpya
Askofu mkuu Luis Antonio Tagle wa Jimbo kuu la Manila, Ufilippini ni kati ya Makardinali
wapya walioteuliwa hivi karibuni na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita kuongeza
nguvu katika huduma ya kufundisha, kutakatifuza na kuwaongoza Watu wa Mungu, inayotolewa
na Khalifa wa Mtakatifu Petro kwa Kanisa la Kiulimwengu; utume ambo unasimikwa katika
mshikamano wa umoja na upendo mkamilifu.Kutujuvya zaidi ndani ya viunga vya Radio
Vatican ni Sr. Gisela Upendo Msuya.
Kardinali
Mteule Luis Antonio Tagle anapenda kuchukua nafasi hii kwanza kabisa kumshukuru Mwenyezi
Mungu na kwa namna ya pekee baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, kwa kumpatia
dhamana ya kushirikiana naye kwa karibu katika kuliongoza Kanisa. Kuteuliwa kwake
ni changamoto endelevu kwa Kanisa Barani Asia kuzidisha juhudi za Uinjilishaji Mpya
unaojikita katika majadiliano ya kidini na kiekuemene, kwa kutambua na kuthamini mchango
mkubwa unaoendelea kutolewa na Kanisa Katoliki nchini Ufilippini.
Kila mwamini
anapaswa kutambua dhamana ambayo amekabidhiwa na Mama Kanisa ya kujikita kwa njia
ya ushuhuda wa maneno lakini zaidi wa matendo yake katika utangazaji wa Habari Njema
ya Wokovu hadi miisho ya dunia.
Kardinali mteule Luis Antonio Tagle katika
barua yake ya kichungaji kwa ajili ya Maadhimisho ya Mwaka wa Imani uliotangazwa na
kuzinduliwa na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, utakaohitimishwa kwa maadhimisho
ya Siku kuu ya Kristo Mfalme hapo tarehe 24 Novemba 2013 ni mwaliko na changamoto
ya kuadhimisha kwa ari na moyo mkuu zaidi, ile zawadi ya imani waliyoipokea kama kito
cha thamani kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kwa kuiishi na kuitangaza kwa njia ya ushuhuda
wa maisha yenye furaha ya kukutana na Kristo.
Mwaka wa Imani una utajiri mkubwa
unaowasukuma waamini kwa namna ya pekee, kujichotea utajiri unaoendelea kububujika
kutoka katika Nyaraka Kumi na Sita za Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican; Muhtasari wa
Imani ambayo waamini wanakiri, adhimisha, wanajitahidi kuiishi na kuisali kama inavyofafanuliwa
na Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki. Ni changamoto ya kuendeleza Mapokeo ya Kanisa
kabla na baada ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican kama alivyofafanua Baba Mtakatifu
Yohane wa Ishirini na tatu wakati wa kuzindua maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili
wa Vatican.
Maadhimisho ya Mwaka Imani uwawezeshe waamini kuzama na kuibua
utajiri ambao umefichika katika Nyaraka hizi ambazo kwa hakika ni dira na mwongozo
kwa maisha na utume wa Kanisa katika ulimwengu mamboleo. Hizi ni jitihada za Mama
Kanisa katika kuendeleza mchakato wa Uinjilishaji Mpya unaopania kuamsha tena Imani
ili kukabuiliana na changamoto, matatizo na fursa mbali mbali zinazojitokeza katika
ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia.
Licha ya dhana
ya ukanimungu kuendelea kushamiri kati ya watu, lakini bado kuna kundi kubwa la Vijana
na Maskini wa Roho wenye kiu ya kutaka kusikia Neno la Mungu likitangazwa kwa ari
na nguvu mpya maishani mwao, kwa kusoma alama za nyakati, kutafuta mbinu muafaka,
kusikiliza na kuendelea kujikita katika maisha na utume wa Kanisa.
Kardinali
mteule Luis Antonio Tagle, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Manila katika barua yake ya
kichungaji kwa ajili ya Maadhimisho ya Mwaka wa Imani anabainisha kwamba, Mwenyezi
Mungu ndiye anayemfungulia mja wake mlango wa mahusiano na umoja unaojikita katika
Fumbo la Utatu Mtakatifu ili kuanza hija ya maisha ya kiroho inayoyojidhihirisha katika
Kanisa ambalo kimsingi ni: Jumuiya ya Waamini na Tunda la kazi ya Roho Mtakatifu,
inayowahamasisha Wafuasi wa Kristo kujitoa kimasomaso kuendeleza utume wa Kimissionari
kwani Kanisa lipo kwa ajili ya Kuinjilisha.
Ili waamini waweze kuishuhudia
Imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, hawana budi kwanza kabisa kuwa na ufahamu wa
kina kuhusu Biblia, dhamana inayoweza kuboreshwa kwa kukazia utume wa Biblia miongoni
mwa waamini, ili kila mtu aweze kuonja utamu wa Neno la Mungu ambalo linapaswa kuwa
ni mwanga na taa inayoyaangazia mapito ya waamini katika hija ya maisha yao hapa duniani.
Waamini waifahamu kwa kina na mapana Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki. Waendelee
kuvumbua utajiri wa Mafundisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican na Nyaraka mbali
mbali ambazo zinaendelea kutolewa na Viongozi wa Kanisa. Mwaka wa Imani, uwawezeshe
waamini kuadhimisha Sakramenti za Kanisa kwa furaha, imani na uchaji na kamwe lisiwe
ni jambo la mazoea ya kushiriki Liturujia na Maisha ya Sala.
Mwaka wa Imani
uoneshe mwamko na ari kubwa zaidi ambayo ni matunda ya toba na wongofu wa ndani, unaopania
kwa namna ya pekee, kujenga utakatifu kama kielelezo cha juu kabisa cha uhusiano kati
ya Mwamini na Muumba wake. Yote haya yajidhihirishe katika maisha adili, haki, amani,
upendo na mshikamano wa dhati na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Waamini
wajitahidi kukuza na kudumisha Umoja wa Kikanisa kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa;
daima wakijitahidi kujenga Ufalme wa Mungu unaosimikwa katika misingi ya haki, amani
na utulivu.