"Watanzania msiwe vibaraka wa kuchochea vurugu na ghasia!
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema
kuwa hakuna mtu yoyote ama kikundi chochote cha watu kitakachoruhusiwa kuvuruga amani
na utulivu wa Tanzania. Aidha, Rais Kikwete amewataka wananchi kuepukana na mtego
wa kufanywa kaseti na gramafoni ya watu wengine katika mchakato wa sasa wa kutoa maoni
kwa ajili ya Katiba Mpya ya Tanzania.
Rais Kikwete ameyasema hayo Alhamisi,
Novemba Mosi, mwaka 2012, wakati alipozungumza na wananchi wa Wilaya ya Arumeru, Mkoa
wa Arusha, baada ya kuwa amefungua rasmi hospitali ya Serikali ya Olturumet nje kidogo
ya mji wa Arusha.
Rais Kikwete amewaambia wananchi hao kuwa mambo ya fujo ambayo
yamejitokeza nchini katika wiki za karibuni ni mambo ya aibu na ya kuchukiza. “Yaliyotokea
na yanayoendelea kuonyesha dalili za kujitokeza ambako watu wanafanya fujo ni mambo
ya aibu na ya kuchukiza. Wapo watu wanaotumiwa ili kuvuruga amani ya nchi yetu kwa
sababu siyo kila mtu anafurahia utulivu ulioko hapa nchini.”
Ameongeza Rais
Kikwete: “Lakini wananchi msiwe na wasiwasi, sisi tutashughulika na hawa watu na kwa
kweli hakuna mtu yoyote ama kikundi cha watu kitakachoruhusiwa kuvuruga amani na utulivu
wa Tanzania.” Hivi karibuni hasa katika Jiji la Dar es Salaam na Zanzibar, zimejitokeza
fujo zilizopelekea watu kadhaa kutiwa mbaroni na Polisi na kufikishwa mahakamani.
Kuhusu
mchakato wa Katiba Mpya, Rais Kikwete amewataka wananchi kuwa huru kutoa maoni yake
mbele ya wajumbe wa Tume ya Katiba. Amewaambia wananchi: “Toeni maoni yenu kwa uhuru
kabisa, msitishwe na mtu yoyote. Jambo moja tu nataka kulisema – msigeuke kuwa kaseti
ama gramafoni za kutangaza na kunadi maoni ya mtu mwingine. Hii ndiyo njia itakayotuwezesha
sote kupata Katiba nzuri na itayoitumikia nchi yetu kwa miaka mingi ijayo.”