2012-11-02 08:07:54

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya 31 ya Kipindi cha Mwaka wa Kanisa: Amri ya Upendo kwa Mungu na Jirani ni muhtasari wa mafundisho makuu ya Yesu!


Mpendwa mwana wa Mungu unayenisikiliza katika kipindi tafakari Neno la Bwana, leo tunatafakari masomo ya Dominika ya 31 ya mwaka B wa Kanisa. Masomo haya yatutaka kutambua wajibu wetu wa msingi ni KUMPENDA MUNGU na JIRANI, yaani kutimiza amri kuu ya mapendo ulio ufupisho wa amri zote na maisha yetu yote kwa ujumla wake. RealAudioMP3

Katika somo la kwanza toka katika kitabu cha Kumbukumbu la Torati, mwaliko kwetu ni kuwa waaminifu katika kushika sheria ya Bwana na kuweza kuwafundisha wengine kuishika sheria hiyo. Katika mwaka huu tunapoadhimisha na kutafakari juu ya imani yetu yafaa kuwaalika wengine na kuwafundisha wema wa Mungu uliotujia kwa njia ya Yesu Kristo Masiha.

Ili tuweze kusadiki na kuamini kina, tunahitaji kuwa na hofu ya Kimungu daima “fear of God”. Hii ina maana ya kujitoa kiaminifu na kujitosa kumtegemea Mungu katika kila jambo na kwa namna hiyo kutimiza mapenzi yake. Hofu ya Kimungu ni upendo thabiti kwa Mungu na kwa jirani. Ni kukubali mpango wa Mungu ambao ndani mwake yeye hujidhihirisha.

Mpendwa msikilizaji, tunaendelea na sehemu ya Barua kwa Waebrania na msisitizo ni ukuhani mkuu wa Yesu Kristo masiha. Mwandishi anazidi kusistiza tofauti iliyopo kati ya ukuhani wa Kristo na makuhani wa Agano la Kale. Jambo la kwanza yeye peke yake anajitosheleza na anatosheleza tangu mwanzo na kabla ya nyakati na baada ya nyakati.

Yeye hana doa la dhambi na pia alingia mara moja madhabahuni kuotolea sadaka na sadaka yake hutosheleza milele, tofauti na makuhani wengine walio na dhambi ambao wanahitaji kuingia mara nyingi katika kutolea dhabihu kwa ajili ya dhambi zao na za wengine. Kumbe, mwandishi anawafundisha Waebrania na sisi kwa wakati wetu kumtazama Yesu Kristo, Kuhani Mkuu wa Agano Jipya na la milele.

Sehemu ya Injili ya Marko, inasisitiza amri kuu ya mapendo yaani kumpenda Mungu na jirani. Kwanza tunaalikwa kuweka nguvu zetu zote katika kumpenda Mungu na kisha tokea huko tutapata fadhili na nguvu mpya za kumpenda jirani yetu. Katika kitabu cha mwanzo Mungu alimwuumba mtu katika sura na mfano wa Mungu na hivi amri ya kumpenda Mungu haiwezi kuachana na upendo kwa jirani vinginevyo Mungu angekuwa akijipinga mwenyewe.

Ni kwa jinsi hiyo katika Injili, Mwenyezi Mungu anatukumbusha lilelile alilokwishatuambia hapo mwanzo. Mialiko hii miwili haipingani bali dhihirisho la upendo uleule wa Kimungu kwa ajili ya mwanadamu, ambaye sasa anaalikwa kurudisha fadhila kwa Mungu. Kwa hakika Mwinjili Yohane anayesema pendaneni kama nilivyowapenda mimi anataka kutuambia tukimpenda jirani tutakuwa tunampenda Mungu.

Ninakutakia furaha na matumaini katika kushika Mafundisho ya Bwana aliye Masiha mteswa kwa ajili ya kumpenda mwanadamu na hatimaye ukombozi wake.

Tumsifu Yesu Kristo.

Tafakari hii imeletwa kwako na Pd. Richard Tiganya, C.PP.S.









All the contents on this site are copyrighted ©.