2012-11-02 09:36:34

Tafakari kuhusu maisha ya uzima wa milele!


Padre Federico Lombardi, Msemaji mkuu wa Vatican katika tahariri yake juma hili, anauangalia kwa namna ya pekee Mwezi Novemba, ambao umetengwa rasmi na Mama Kanisa kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea waamini marehemu. Ni mwaliko wa kuyainua macho mbinguni kwa imani na matumaini juu ya ufufuko wa wafu na uzima wa milele ijayo.

Macho ya waamini yanatamani kuiona Jumuiya ya wale waliokombolewa, yaani watakatifu wanaoendelea kufurahia utukufu wa Mungu katika maisha ya uzima wa milele; waamini wanatumaini la kuonja umoja wao katika maisha ya kiroho, waamini wanapoendelea na hija ya maisha yao kuelekea mbinguni. Hii ndiyo maana ya Sherehe ya Watakatifu Wote, ambayo Mama Kanisa ameiadhimisha hapo tarehe Mosi, Novemba.

Waamini wanaonesha mshikamano wao wa kiroho na waamini waliotangulia mbele za haki kwa kuwakumbuka katika sala na matumaini. Mababa wa Sinodi ya Maaskofu juu ya Uinjilishaji Mpya, katika ujumbe wao kwa Watu wa Mungu wanasema kwamba, Yesu alipokutana na yule mwanamke Msamaria alijionesha si tu kwamba, ni mtu anayetoa maisha, bali zaidi sana ni mtu anayemkirimia mwanadamu maisha ya uzima wa milele.

Padre Lombardi anasema kwamba, zawadi hii kutoka kwa Mwenyezi Mungu hajikiti katika ahadi ya maisha bora hapa ulimwenguni, lakini ni ujumbe unaolenga katika hatima ya maisha ya mwanadamu baada ya kifo, yaani muungano mkamilifu na Mwenyezi Mungu, jambo ambalo waamini wanalisubiri hadi utimilifu wa dahali.

Ujumbe wa Mababa wa Sinodi unaendelea kukazia kwamba, kwa wale ambao wamewekwa wakfu kwa ajili ya Mungu na jirani, katika nadhiri ya ufukara, useja na utii, wanapaswa kuwa kweli ni kielelezo cha matumaini ya maisha ya binadamu yanayopita mipaka ya kifo. Ni wito angavu lakini una madai yake makubwa!

Utekelezaji wa majukumu hapa duniani ni haki na jambo muhimu kabisa, lakini hauna budi kulishwa na kuchangamotishwa na tumaini linaloelekea kwenye mbingu na dunia mpya. Padre Federico Lombardi anahitimisha tahariri yake kwa kusema kwamba, bila tumaini hili, dhamana ya Uinjilishaji wa awali ingegonga mwamba na wala kusingalikuwepo na ndoto kuhusu Uinjilishaji Mpya. Ni vyema, kwa waamini kuviinua vichwa vyao, ili kumwangalia Kristo anayekuja akiwa na jeshi kubwa la watakatifu.







All the contents on this site are copyrighted ©.