Mwilisheni Injili ya Upendo kwa kuwahudumia maskini, wagonjwa na wote wanaokosa hakimsingi
za kijamii!
Kardinali Thèodor Adrien Sarr, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dakar, Senegal, katika
maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu wote, anaendelea kuwaalika waamini na watu wote
wenye mapenzi mema, kujitahidi katika hija ya maisha yao hapa duniani kuhakikisha
kwamba, wanamwilisha Injili ya Upendo kwa waathirika wa majanga asilia, umaskini,
magonjwa, ujinga na ukosefu wa misingi ya haki jamii.
Ni sherehe inayopaswa
kuacha chapa ya kudumu katika maisha ya waamini, kwani kila mwamini anachangamotishwa
na Mama Kanisa kuwa ni mtakatifu, mwaliko wa kwanza kabisa kutolewa na Kristo mwenyewe.
Maisha na majina ya watakatifu yasibaki kwenye Kalenda zilizotundikwa ukutani au vitabu
vilivyofichwa kwenye makabati, bali yawe ni maisha halisi yanayojionesha katika hija
ya waamini hapa duniani.
Ni safari ya kiroho inayopaswa kufanyika kwa kukumbatia
kwa namna ya pekee: unyenyekevu, uvumilivu na utu wema, daima wakipania kujenga na
kudumisha misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano wa dhati. Fadhila hizi zinapaswa
kuwa ni chimbuko la upatanisho, msamaha na furaha ya ndani inayobubujika kutoka kwa
Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu, limbuko lao waliolala katika
maisha ya uzima wa milele.
Kardinali Sarr kwa namna ya pekee, ameichangamotisha
Serikali ya Senegal kuhakikisha kwamba, inawatia mbaroni na kuwafikisha kwenye mkondo
wa sheria, watu waliofanya vitendo vya kihuni kwa kubomoa makaburi ya Wakristo nchini
Senegal hivi karibuni, kwani makaburi ni maeneo matakatifu yanapaswa kuheshimiwa na
kuhifadhiwa na kila raia, kwani hii ni nyumba ya kila mwanadamu.