Yesu Kristo Mwanga wa Mataifa ajioneshe katika: Liturujia, Neno la Mungu, Kanisa na
katika Ulimwengu
Mababa wa Sinodi ya Maaskofu juu ya Uinjilishaji Mpya katika Ujumbe wao kwa Familia
ya Mungu wanabainisha kwamba, fursa mbali mbali zinazotolewa na Mama Kanisa katika
Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, Kumbu kumbu ya Jubilee ya Miaka hamsini ya Mtaguso
Mkuu wa Pili wa Vatican na Miaka ishirini tangu Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili,
alipochapisha Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki, ziwe ni fursa makini katika azma
ya Uinjilishaji Mpya.
Kwa namna ya pekee, Mababa wa Sinodi wanakazia umuhimu
wa Liturujia katika maisha na utume wa Kanisa, kama chechemi ya imani na mahali ambapo
panapaswa kupewa kipaumbele cha pekee katika kuiungamana, kuitangaza na kuimwilisha
Imani ya Kikristo. Liturujia ya Neno la Mungu ilete changamoto ya pekee kwa waamini
kupenda kulitafakari, kulisoma na kulimwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha
yao.
Daima wakumbuke kwamba, Neno hili halina budi kupokelewa katika hali
ya utulivu, kumwilishwa kwa njia ya huduma kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni
mwa Jamii, ili kutambua ile sura ya Kristo mteswa inayojionesha miongoni mwa ndugu
zake walio wadogo.
Katika mahojiano maalum na Radio Vatican, Askofu Salutaris
Libena wa Jimbo Katoliki Ifakara ambaye alikuwa ni kati ya Mababa wa Sinodi ya Maaskofu
juu ya Uinjilishaji Mpya anabainisha umuhimu wa Liturujia katika maisha na utume wa
Kanisa kwa kufanya rejea kutoka katika Waraka wa Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi
na sita, katika maadhimisho ya Mwaka wa Imani "Porta Fidei" "Mlango wa Imani"
kwamba, Mwaka huu, waamini wajitahidi kumtambua Kristo Mwanga wa Mataifa anayejionesha
kwa namna ya pekee kabisa katika Liturujia, Maandiko Matakatifu, Kanisa na Katika
Ulimwengu.
Kimsingi huu ni muhtasari wa Mafundisho Makuu ya Mtaguso Mkuu wa
Pili wa Vatican yanayofumbatwa katika Nyaraka zifuatazo: Liturujia, Maandiko Matakatifu,
Kanisa na Ulimwengu. Kwa njia ya Liturujia, waamini wanaweza kumtukuza, kumshukuru,
kumwomba, kumsifu na kumwabudu mwenyezi Mungu kwa njia ya Neno lake, Sakramenti za
Kanisa, Matendo ya Huruma, Umoja na Mshikamano miongoni mwa Wafuasi wa Kristo. Waamini
wakiweza kuitambua na kuiishi Liturujia ya Kanisa.