2012-11-01 09:43:41

Michoro ya Kikanisa cha Sistina ni mwaliko wa kusali na kutafakari ili kugundua utajiri unaofumbatwa katika michoro hii


Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, Jumatano tarehe 31 Oktoba, 2012 ameongoza waamini katika maadhimisho ya Masifu kwa ajili ya Watakatifu Wote sanjari na Jubilee ya miaka mia tano tangu Baba Mtakatifu Giulio wa Pili alipozindua Michoro iliyopo kwenye Kikanisa cha Sistina.

Tukio hili la kihistoria na kisanii limeadhimishwa katika Liturujia kwa kutambua umuhimu wa Kikanisa cha Sistina katika maisha na utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Michoro iliyopo inapata chimbuko lake katika Liturujia ya Kanisa na uzuri wake unajionesha kwa namna ya pekee kabisa, kwani maadhimisho ya Kiliturujia yanakwenda sanjari na uzuri unaogusa undani wa maisha ya mwamini kiroho. Kwa maneno machache anasema Baba Mtakatifu, michoro ya Kikanisa cha Sistina ni mwaliko wa kusali na kufanya tafakari ya kina ili kugundua utajiri unaofumbatwa katika michoro hii.

Baba Mtakatifu anasema, Liturujia ya Neno la Mungu inawakumbusha waamini kwamba, Ahadi za Agano la Kale zilizotolewa na Mwenyezi Mungu zinatoa kipaumbele cha kwanza kwa waamini hao kujenga umoja na mshikamano: Mwenyezi Mungu na Kristo wakiwa ni kiini cha maadhimisho yao. Michoro iliyoko kwenye Kikanisa cha Sistina inaonesha Jumuiya ya Watakatifu, Bikira Maria, Mama wa Matumaini, Yesu Kristo Mkombozi wa Ulimwengu akiwa kati kati kabisa ya michoro yote, hali akiwa amezungukwa na Jeshi la Watakatifu.

Msanii Michelangelo alipewa dhamana ya kuchora kwenye Kikanisa cha Sistina na Papa Giulio wa Pili, kazi ambayo aliitekeleza kwa kipindi cha miaka minne, kuanzia mwaka 1508 hadi mwaka 1512, michoro ambayo inamguso wa pekee kwa mtu anayetembelea Kikanisa hiki.

Ni michoro iliyoleta mabadiliko makubwa katika historia ya sanaa ya Italia na kwa Bara la Ulaya katika ujumla wake, kwani huu ni mwanga unaoiangazia dunia kutokana na uzuri wake. Ni mwanga wa Mungu unaoangazia michoro iliyomo kwenye Kikanisa cha Sistina na kuwa ni chemchemi inayobubujikia maisha mapya yanayojikita katika kazi ya uumbaji na ukombozi.

Michoro hii ni kielelezo cha kazi ya Ukombozi; inaonesha uhusiano kati ya Mwenyezi Mungu na Mwanadamu. Ni picha zinazodhihirisha: nguvu, utukufu na ukuu wa Mungu katika kazi ya Uumbaji ambayo ni matunda ya uhuru kamili na upendo wa dhati kabisa kutoka kwa Mwenyezi Mungu; inaunganisha mbingu na dunia. Kwa njia ya Adamu, Mwenyezi Mungu anaanzisha uhusiano mpya na kazi ya Uumbaji, kwa vile mwanadamu ameumbwa kwa sura na mfano wake, anakuwa na uhusiano wa moja kwa moja na Muumba wake.

Baba Mtakatifu anasema, Msanii maarufu Michelangelo, baada ya miaka ishirini, aliweza kukamilisha kazi hii kubwa inayoonesha Siku ya Hukumu, Yesu atakapokuja kuwahukumu wazima na wafu na kwamba, Ufalme wake hautakuwa na mwisho.

Maadhimisho ya Masifu katika Kikanisa cha Sistina kinachosheheni michoro mbali mbali ni kuonesha hija ambayo Mwenyezi Mungu anaendelea kufanya na binadamu, changamoto kwa waamini kupaza sauti zao kwa Mwenyezi Mungu: Muumbaji, Mkombozi na Hakimu wa wazima na wafu pamoja na zile za watakatifu wote kwa kusema, Amina, Alleluiya.







All the contents on this site are copyrighted ©.