Kila mwamini anaitwa kuchuchumilia utakatifu, yaani maisha ya uzima wa milele katika
utukufu wa Kristo
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, katika maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu
Wote, Alhamisi, tarehe Mosi Novemba, 2012, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu
Petro, mjini Vatican, anasema hii ni Sherehe inayoonesha hija ya kihistoria inayopata
utimilifu wa maisha yake kwa Mwenyezi Mungu.
Hiki ni kielelezo cha Kanisa
linalosafiri katika nyakati na Kanisa ambalo tayari limekwishafikia utimilifu katika
Yerusalemu ya mbinguni, ukweli unaojionesha katika umoja na watakatifu, hija ya maisha
ambayo yalianza hapa duniani na hatimaye, kufikia hitimisho lake mbinguni.
Hapa
duniani, Kanisa limeanzisha Fumbo la Umoja kwa kuwakusanya watu wote ili kuwapeleka
kwa Mwenyezi Mungu, wakati huo huo, likishughulikia mshikamano na amani. Yesu aliteswa,
akafa na kufufuka ili kuwaunganisha watoto wa Mungu waliotawanyika sehemu mbali mbali
za dunia katika utume huu unaotekelezwa na Kanisa ambalo ni: Moja, Takatifu na Katoliki.
Wakristo
ni sehemu ya Kanisa ambalo kimsingi linajifunua kwa ajili ya kudumisha umoja huu,
ili kufikia maisha mapya yanayopata utimilifu wake mbinguni. Watakatifu ni watu ambao
walijitahidi kuuishi ukweli huu, kwa njia ya Roho ya Kristo inayojidhihirisha katika
Neno la Mungu na Sakramenti za Kanisa.
Ni watu wanaounganishwa na upendo kwa
Kristo na Kanisa lake na hivyo kuwa kweli ni sura ya Mwana wa Mungu daima wakiendelea
kutekeleza ule mpango wa Mungu wa kumuumba mwanadamu, kwa sura na mfano wake; ni umoja
unaofumbata wote wanaounda Fumbo la Mwili wa Kristo katika umoja kamili.
Sherehe
ya Watakatifu wote anasema Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, inawawezesha
waamini kuonja maisha ya uzima wa milele wakiwa na mtazamo wa upendo wa Mungu na jirani,
ili kwa pamoja kuweza kumfikia Mwenyezi Mungu na jirani. Kwa njia ya imani hii, waamini
wote wanajawa matumaini ya kuwa ni watakatifu na hivyo kujiandaa kuadhimisha Siku
ya Kuwakumbuka Marehemu wote, inayoadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo hapo
tarehe 2 Novemba.
Katika maisha ya watakatifu, waamini wanaona ushindi wa upendo
dhidi ya ubinafsi na kifo; wanachangamotishwa kumfuasa Kristo ambaye ni mlango wa
maisha ya uzima wa milele na anatoa maana halisi ya maisha yanayosheheni upendo na
matumaini.
Imani katika maisha ya uzima wa milele inawawezesha waamini anasema
Baba Mtakatifu kupenda historia na hali ya maisha ya sasa bila ya kujishikamanisha
na malimwengu, lakini katika uhuru kamili kwa kutambua kwamba, wao ni mahujaji wanaoipenda
dunia, lakini moyo wao umejikita zaidi kwa mambo ya mbinguni.