Maadhimisho ya Siku kuu ya Watakatifu Wote na Marehemu Wote yawawezeshe waamini kuwa
kweli ni Mashahidi wa Upendo wa Mungu kwa watu wake!
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, Jumatano, tarehe 31 Oktoba 2012, katika
katekesi yake kama sehemu ya Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, anasema kwamba: imani
inapaswa kuwa ni sehemu ya undani wa maisha ya mtu: hii ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi
Mungu inayomletea mwamini mabadiliko na utajiri mkubwa katika maisha ya kiroho.
Imani
ni zawadi inayotolewa kwa njia ya Jumuiya ambayo ni Kanisa. Katika Ubatizo, mwamini
anapokea zawadi ya imani na kuimwilisha katika maisha yake ya kila siku ndani ya Kanisa;
imani ambayo kimsingi ni zawadi kwa mtu binafsi inajidhihirisha katika kusali Kanuni
ya Imani na pale mwamini anaposhiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Sakramenti
za Kanisa.
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita anasema kwamba, hii ni
chemchemi ya maisha mapya, inayomwezesha mwamini kwa njia ya Kristo na kwa kupitia
Roho wake aliyempokea na kuendelea kuboreshwa kwa njia ya umoja ndani ya Kanisa. Kutokana
na mwelekeo huu, Kanisa ni Mama ya Waamini, kama alivyowahi kusema Mtakatifu Cyprian
kwamba, hakuna mtu anayeweza kujigamba kwamba Mwenyezi Mungu ni Baba yake bila kuzingatia
kwamba, Kanisa ni Mama yake pia.
Ndani ya Kanisa kuna hifadhi kubwa ya Mapokeo
Hai. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuhakikisha kwamba, wanakua na kukomaa katika
misingi ya imani waliyoipokea kutoka kwa Mama Kanisa na kwa kuimwilisha katika uhalisia
wa maisha, basi waamini hawa waweze kuwa kweli ni nuru ya mwanga wa Kristo na amani
ya dunia.
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, ametumua fursa hii kutoa
pole kwa wote walioathirika kutokana na kimbunga kilichoikumba Marekani katika siku
za hivi karibuni na hivyo kusababisha maafa na uharibifu mkubwa wa mali na miundo
mbinu. Baba Mtakatifu anapenda kuwahakikishia uwepo wake wa karibu kwa njia ya sala,
hasa kipindi hiki kigumu cha historia ya maisha yao. Anapenda kuwatia moyo pamoja
na kuwaonesha mshikamano wake wale wote wanaojishughulisha katika ukarabati na ujenzi
mpya wa maeneo yaliyokumbwa na tufani hii.
Baba Mtakatifu amewatakia kheri
na baraka mahujaji na wageni kutoka katika nchi zinazozungumza lugha ya Kiingereza
waliohudhuria Katekesi yake siku ya Jumatano, lakini kwa namna ya pekee kabisa, mahujaji
kutoka Nigeria wanaotembelea mji wa Roma kwa wakati huu.
Baba Mtakatifu pia
ametumua fursa hii kwa ajili ya kuwashukuru waamini wote waliojibidisha kusali Rozari
Takatifu wakati wa Mwezi Oktoba, uliotengwa maalum kwa ajili ya Rozari Takatifu, muhtasari
wa maisha ya Yesu. Anawashukuru kwa kuwaombea Mababa wa Sinodi ya Maaskofu iliyohitimishwa
hivi karibuni kama sehemu ya maadhimisho ya Mwaka wa Imani.
Maadhimisho ya
Siku kuu ya Watakatifu wote pamoja na kumbu kumbu ya Marehemu Wote yawe ni matukio
yatakawasaidia waamini kuwa mashahidi wa upendo wa Mungu.
Baba Mtakatifu anawapongeza
Wanachama wa Umoja wa Vijana Wakatoliki Italia wanapoadhimisha miaka mia moja tangu
umoja huu ulipoanzishwa kwa hakika, umekuwa na manufaa makubwa kwa Kanisa mahalia.
Baba Mtakatifu ametambua uwepo wa Wakuu wa Vyuo Vikuu na Taasi za Elimu ya
Juu zinazosimamiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki wanaoendelea na mkutano wao hapa
mjini Roma. Anasema, uwepo wao hapa Roma, ukuze imani yo kwa Kristo na Kanisa lake.