2012-10-30 06:57:47

Watu 10 wafariki dunia na wengine 145 wamejeruhiwa vibaya Kaduna, nchini Nigeria kutokana na mlipuko wa bomu la kujitoa mhanga!


Viongozi mbali mbali wa Kanisa na Serikali nchini Nigeria, kwa mara nyingine tena wamelaani vitendo vya kinyama vinavyoendea kufanyika nchini Nigeria kwa kuchoma Makanisa.

Jumapili iliyopita, tarehe 28 Oktoba 2012, watu kumi walipoteza maisha yao na wengine mia moja na robaini na tano kujeruhiwa vibaya sana kutokana na vitendo vya kigaidi vinavyoendelea kufanywa na Kikundi cha Boko Haram, hali iliyopelekea baadhi ya Wakristo nao kutaka kulipiza kisasi baada ya kuchoshwa na madhulumu haya yenye mwelekeo wa kidini.

Hayo yametokea huko Kaduna, Nigeria, baada ya mtu mmoja kujitoa mhanga na hatimaye kulipua Kanisa la Mtakatifu Rita, Jimbo kuu la Kaduna, wakati waamini walipokuwa wanaadhimisha Ibada ya Misa Takatifu. Mlipuko huo wa bomu umesababisha hasara kubwa kwa majengo yaliyo karibu na Kanisa la Mtakatifu Rita.

Akizungumzia kuhusu tukio hili, Rais Goodluck Jonathan wa Nigeria anasema kwamba, hivi ni vitendo vya kinyama ambavyo haviwezi kuvumiliwa kamwe. Ni changamoto kwa Nigeria kuendelea kuwekeza zaidi katika ulinzi na usalama kwa raia na mali zao. Vitendo vya kigaidi vinaendelea kuhatarisha misingi ya amani, utulivu na umoja wa kitaifa nchini Nigeria.

Kwa upande wake, Askofu mkuu Mathew Man-oso Ndagoso wa Jimbo kuu la Kaduna, Nigeria, anawaalika waamini na wananchi wote kwa ujumla kutulizana ili kuepuka vitendo vya kulipizana kisasi vinavyoweza kusababisha athari kubwa kwa wananchi wa Nigeria.

Ameitaka Serikali kuhakikisha kwamba, inawajengea raia wake mazingira ya amani na utulivu. Ni matumaini ya Askofu mkuu Ndagoso kwamba, viongozi mbali mbali wa dini ya Kiislam wataunga mkono jitihada za kujenga amani na utulivu kwa kulaani vitendo vya kigaidi dhidi ya watu wasiokuwa na hatia.







All the contents on this site are copyrighted ©.