Uhusiano wa Kidiplomasia kati ya Vatican na Croatia unafumbata utajiri wa kijiografia,
kihistoria na kidini
Askofu mkuu Dominique Mamberti, Katibu mkuu wa Mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa
mjini Vatican, katika maadhimisho ya miaka ishirini tangu Croatia ilipoanzisha uhusiano
wa kidiplomasia, hapo tarehe 29 Oktoba, 2012 amegusia kwa namna ya pekee, utajiri
wa kijiografia, kihistoria na kidini unaofumbatwa katika mahusiano ya kidiplomasia
kati ya Vatican na Croatia.
Katika historia ya nchi ya Croatia, daima imejitahidi
kuonesha uaminifu kwa Injili ya Kristo na Khalifa wa Mtakatifu Petro, kama Baba Mtakatifu
Benedikto wa kumi na sita, alivyobainisha wakati wa hija yake ya kichungaji nchini
Croatia, kunako mwaka 2011.
Hili ni taifa ambalo limechangia kwa kina na mapana
katika kulinda na kudumisha tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kimaadili sanjari
na kutoa utambulisho kwa watoto wake. Ilikuwa ni tarehe 13 Januari 1992 Croatia ilipotambuliwa
na Vatican kuwa ni taifa huru na tangu wakati huo, mchakato wa uhusiano wa kidiplomasia
baina ya pande hizi mbili ukaanza katika njanja za: kisheria, elimu, utamaduni, huduma
za kiroho kwa vikosi vya ulinzi na usalama pamoja na uchumi.
Askofu mkuu Mamberti
anasema kwamba, kumekuwepo na maendeleo makubwa katika kudumisha uhusiano wa kidiplomasia
kati ya Vatican na Croatia; hasa kwa kukuza majadiliano kati ya viongozi wa Kanisa
na Serikali pamoja na Croatia kuendelea kuchangia katika ustawi na maendeleo ya Jumuiya
ya Kimataifa.
Amewashukuru viongozi mbali mbli wa Kanisa na Serikali walioendelea
kuboresha uhusiano huu wa kidiplomasia katika kipindi cha miaka ishirini iliyopita,
jambo ambalo limepanua na kuendeleza majadiliano na ushirikiano, huduma pamoja na
kusimama kidete kulinda, kutetea haki msingi za binadamu, utu na heshima ya binadamu;
daima wakitafuta mafao ya wengi pamoja na kuendeleza tunu msingi za maisha ya kiroho
na kimaadili.