2012-10-30 09:35:08

Kanisa limekuwa mstari wa mbele kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji katika maisha yao ya kiroho na kimwili


Kardinali Antonio Maria Veglio na Askofu mkuu Joseph Kalathiparambili, Rais na Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Wahamiaji na Watu wasiokuwa na makazi maalum, Jumatatu, tarehe 29 Oktoba 2012, waliwasilisha kwa waandishi wa habari ujumbe wa Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita kwa ajili ya maadhimisho ya Siku ya Wakimbizi Duniani itakayoadhimishwa hapo tarehe 13 Januari 2013 kwa kuongozwa na kauli mbiu " Uhamiaji: Hija ya Imani na Matumaini".

Kardinali Veglio anasema kwamba, Kanisa limekuwa m stari wa mbele kuwahudumia wakimbizi kwa hali na mali, wakimbizi ambao kadiri ya takwimu za Umoja wa Mataifa kwa Mwaka 2011 wamefikia kiasi cha watu millioni mia mbili na kumi na nne. Taarifa inaonesha pia kwamba, katika kipindi cha Mwaka 201o kulikuwa kuna jumla ya watu wasiokuwa na makazi wapatao millioni mia saba na arobaini, waliokuwa wameenea sehemu mbali mbali za dunia.Takwimu hizi zinaonesha jinsi ambavyo uhamiaji ni tatizo na changamoto kubwa kwa Jumuiya ya Kimataifa.

Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, anasema katika ujumbe wake, wahamiaji ni mahujaji wanaobeba ndani mwao imani na matumaini, hata kama hawafahamu kwa kina na mapana kile wanachotafuta katika hija ya maisha yao. Ni watu wanaopania kuboresha hali yao ya uchumi na kijamii, wakiwa na matumaini kwamba, Mwenyezi Mungu kamwe hatawaacha katika shida na mahangaiko yao ya kila siku. Ni watu ambao wakiwezeshwa, wanaweza kugundua uwepo wa Mungu na Kanisa katika hija ya maisha yao ya kiimani, kwa njia ya ukarimu na huduma makini zinazotolewa kwa wahamiaji na wakimbizi.

Kutokana na changamoto hizi, Mama Kanisa anaalikwa kwa namna ya pekee, kuhakikisha kwamba, anawaonjesha huruma na upendo wake wa Kimama, Wakimbizi na Wahamiaji, kwa kuibua mbinu mkakati utakaowawezesha wahamiaji kuhudumiwa kikamilifu kutokana na kukabiliwa na hali ya hatari. Jambo la pili ni kuwasaidia wananchi kubadili mwelekeo wao dhidi ya wahamiaji na wakimbizi, kwa kuhakikisha kwamba, wanasaidiwa kuingia katika mfumo wa maisha ya kijamii na kitamaduni za watu wanaowakirimia.

Kardinali Veglio anasema kwamba, ujumbe huu unatolewa na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, mara tu baada ya kurudi kutoka kwenye hija yake ya kichungaji huko Lebanoni, ambako, mawazo na macho ya Kanisa yanaweza kuelekezwa zaidi kwa kundi kubwa la Wakristo wanaolazimika kuzikimbia nchi zao kutokana na sababu mbali mbali, kiasi cha kujikuta wanalazimika kuishi katika tamaduni na mitindo mipya ya maisha pamoja na kuhamasishwa kuunda uhusiano mpya na wenyeji wao.

Mama Kanisa kwa miaka mingi amekuwa mstari wa mbele kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji katika maisha yao: kiroho na kimwili pamoja na kuwajengea uwezo wa kujiunga kikamilifu na Jamii inayowazunguka. Mama Kanisa anatekeleza dhamana hiii, akipania kulinda, kutetea na kudumisha utu na heshima ya kila mtu; kuwatetea na kuwalinda wanawake na watoto; daima akithamini mchango wao unaobubujika kutoka katika tamaduni na mapokeo yao katika mchakato mzima wa ujenzi wa utamaduni wa amani, mwelekeo wa kimissionari pamoja na kukuza umuhimu wa majadiliano ya kijamii, kidini na kiekumene.

Mama Kanisa anatekeleza yote haya akipania kwanza kabisa: kutatua matatizo yanayowakabili wahamiaji na wakimbizi: kijamii, kitamaduni na kiroho, ili watu hawa pia waweze kuona ndani mwao chapa ya utu na ukristo inayotoa dira na mwanga katika hija ya maisha yao ugenini.

Kwa upande wake, Askofu mkuu Joseph Kalathiparambil, amepembua kwa kina na mapana matatizo na changamoto wanazokabiliana nazo wahamiaji na wageni wanaotafuta hifadi ya kisiasa. Baadhi ya wahamiaji na wakimbizi wamekumbana na sheria katili zinazowanyima fursa ya kuingia katika baadhi ya nchi, bila ya kuwa na vibali maalum. Wamejikuta wanakabiliwa na mkono wa sheria na nchi zao kupachikwa kwenye orodha ya mataifa hatari.

Sheria na hatua kama hizi zimepelekea kukua na kupanuka kwa biashara haramu ya binadamu, inayoendelea kuwafaidisha watu wachache katika Jamii pamoja na kudhalilisha utu na heshima ya binadamu. Ni tatizo ambalo limepelekea watu wengi wanaosafirishwa katika biashara haramu ya binadamu kupoteza maisha yao wakiwa njiani kama inavyojionesha kwenye matukio mbali mbali ya kimataifa na kitaifa.

Inasikitisha kuona kwamba, yote haya yanatendeka wakati ambapo Jumuiya ya Kimataifa inalo jukumu na dhamana ya kulinda na kutetea wakimbizi, wahamiaji na wote wanaotafuta hifadhi ya kisiasa mintarafu sheria za kimataifa na haki msingi za binadamu. Waathirika wakubwa ni wale wanaotafuta hifadhi ya kisiasa baadaye, linafuata kundi la watu wanaotafuta mahitaji msingi kama vile: chakula, malazi na huduma za matibabu, bila kusahau haki ya kufanya kazi na kutembea kadiri ya sheria za nchi.

Watu wanaotafuta hifadhi ya kisiasa wanajikuta wakivuka mipaka ya nchi zao na kwamba, wanawajibika kuwa na hati rasmi au vitambulisho vyao, kwani haki na wajibu ni chanda na pete.







All the contents on this site are copyrighted ©.