Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameuelekeza
uongozi wa Mkoa wa Kilimanjaro na hasa Wilaya ya Same kufanya tathmini kamili na ya
haraka kujua kiwango cha njaa katika wilaya hiyo ili kuiwezesha Serikali kutoa chakula
cha msaada ama cha bei nafuu kwa wananchi.
Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa
Serikali yake itaipatia jawabu la kudumu changamoto ya maji katika maeneo ya Mkoa
wa Kilimanjaro na hasa Wilayani Same.
Rais Kikwete alitoa agizo la kushughulikia
tatizo la njaa, Jumatatu, Oktoba 29, 2012, wakati alipoelezwa na wananchi katika maeneo
mbali mbali ya Wilaya ya Same aliposimama mara kwa mara kusalimia wananchi kwenye
siku ya pili ya ziara yake ya siku nne Mkoani Kilimanajaro.
Wananchi katika
maeneo ya Hedaru na Lembeni walimwambia Mheshimiwa Rais Kikwete kuwa wanakabiliwa
na njaa kwa sababu ya ukame ambao umesababisha wasipate chakula cha kutosha kwa miaka
mitatu iliyopita.
Baada ya kusikiliza malalamiko hayo hasa kuhusu njaa na ukosefu
mkubwa wa maji, Rais Kikwete alisema: “Nimesikia maelezo yenu kuhusu ukosefu wa chakula
na njaa. Mkuu wa Mkoa yupo hapa pamoja na Mkuu wa Wilaya na napenda kuwaagiza wafanye
tathmini ya haraka kuhusu kiwango cha tatizo ili Serikali ichukue hatua ya kumaliza
tatizo hili.”
Aliongeza Mheshimiwa Rais: “Hakuna wasiwasi. Hakuna mtu ambaye
atapoteza maisha yake kwa sababu ya njaa. Tunacho chakula cha kutosha na Serikali
itahakikisha chakula kinapatikana mara tu tathmini itakapokamilika.”
Aliongeza
Rais Kikwete: “Chakula kitakuwa cha aina mbili. Kwa familia zisizokuwa na uwezo
kabisa chakula kitatolewa bure. Kwa wale wanaojiweza, chakula kitatolewa kwa wananchi
kuchangia fedha kidogo sana kama Sh. 50 tu.”
Rais Kikwete alisimamishwa mara
tisa na wananchi ambao walikuwa na hamu ya kumwona na kusalimiana naye akiwa njiani
kutoka Mamba Miamba ambako alizindua Kiwanda cha Kusindika Tangawizi kwenda Mwanga
ambako alifungua Hosteli ya Shule ya Wasichana ya Asha Rose Migiro mjini Mwanga.