TAHADHARI YA UGONJWA WA MARBURG AFRIKA YA MASHARIKI
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, imepokea taarifa kutoka Shirika la Afya Duniani
(WHO), tarehe 20 Oktoba, 2012 kuhusu ugonjwa wa Marburg ambao umejitokeza katika nchi
jirani ya Uganda. Maeneo yaliyokumbwa na ugonjwa huo ni Wilaya ya Kabale, Kanda ya
Kusini Magharibi ya nchi, na wilaya hii inapakana na Rwanda. Mpaka tarehe 24 Oktoba
2012, takriban watu 13 wamepata maambukizo na 6 wamepoteza maisha..
Wizara
ya Afya na Ustawi wa Jamii inapenda kutoa tahadhari ya Ugonjwa huu kwa wananchi wote,
katika mikoa yote ya Tanzania na hasa wale waliopo katika mikoa ambayo inapakana na
na nchi jirani ya Uganda (Mikoa ya Mara, Mwanza, Kagera na Kigoma).
Marburg
ni ugonjwa wa hatari unaofanana na Ebola na unasababishwa na virusi vijulikanavyo
kwa lugha ya kitaalam “Marburg Virus”. Ugonjwa huu ni miongoni mwa magonjwa yajulikanayo
kwa ujumla kama Homa za Virusi zinazosababisha kutokwa damu mwilini, (Viral Haemorrhagic
Fevers). Chanzo kamili cha virusi vya ugonjwa huu hakijulikani. Hali inayosababisha
mlipuko wake pia haijulikani. Ugonjwa huu hauna tiba wala chanjo.
Dalili kuu
za ugonjwa huu ni pamoja na Homa kali, inayoambatana na kutokwa damu katika matundu
yote ya mwili yaani pua, njia ya haja kubwa na ndogo, mdomoni, masikioni, machoni,
hali inayopelekea kifo kwa muda mfupi. Kipindi cha kuonekana kwa dalili za ugonjwa
ni kati ya siku 3 hadi 9 baada ya kupata maambukizi.
Ugonjwa huu unaenea kwa
urahisi sana na haraka kutoka mtu mmoja hadi mtu mwingine iwapo mtu atakuwa karibu
na mgonjwa na kugusana na mate, damu, mkojo, machozi, kamasi, maji maji mengine ya
mwili, ikiwa ni pamoja na jasho au kumgusa mtu aliyekufa kwa ugonjwa wa Marburg.Ugonjwa
huu pia unaweza kuenezwa iwapo mtu atagusa nguo au mashuka ya mgonjwa wa Marburg.
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, imechukua hatua zifuatazo katika kukabiliana
na tishio la ugonjwa huu:
Kutoa taarifa ya tahadhari ya ugonjwa huu kupitia
kwa Waganga Wakuu wote wa Mikoa na Wilaya. Aidha taarifa hii pia imejumuisha namna
mgonjwa anavyoweza kutambuliwa (Ainisho la Ugonjwa), “Fact sheet” ya ugonjwa, Mwongozo
kwa watumishi wa afya wa namna ya kuchukua sampuli na vipeperushi vinavyoelezea ugonjwa
huu.
Kuimarisha ufuatiliaji wa ugonjwa huu kupitia kwa Wataalamu wa Afya
katika Mikoa, Wilaya na maeneo ya mipaka. Aidha watalaamu hawa wa Afya pia wanatoa
elimu kwa wananchi kuhusu dalili za ugonjwa huu ili endapo ugonjwa huo utatokea uweze
kutolewa taarifa mapema.
Kupeleka vifaa kinga kwa ajili ya watumishi wa afya
Wananchi wanashauriwa kutokuwa na hofu kwani mpaka sasa hakuna mgonjwa yeyote
aliyeripotiwa nchini. Wananchi wanashauriwa kutoa taarifa kwenye kituo cha huduma
za afya kilicho karibu mara watakapoona mgonjwa yeyote atakayehisiwa kuwa na dalili
za ugonjwa huu.