2012-10-29 07:58:40

Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu ni kielelezo cha nguvu kinachoonesha umoja na mshikamano wa Kanisa zima!


Mara baada ya maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kufunga Sinodi ya Maaskofu juu ya Uinjilishaji Mpya, Jumapili tarehe 28 Oktoba 2012, Baba Mtakatifu aliungana na umati mkubwa wa waamini uliokuwa umekusanyika kwenye Uwanja wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro, kwa ajili ya kusali Sala ya Malaika wa Bwana.

Anasema, kwa takribani majuma matatu, Mababa wa Sinodi wamefanya tafakari ya kina kuhusu hali hali ya Uinjilishaji Mpya kama njia ya kutangaza Imani ya Kikristo. Kanisa zima liliwakilishwa wakati wa maadhimisho haya, kielelezo cha nguvu kinachoonesha kwa namna ya pekee, Umoja wa Kanisa. Ndiyo maana Baba Mtakatifu anapenda kuchukua fursa hii kuungana pamoja na Waamini wote kumshukuru Mungu kwa zawadi kubwa aliyoweza kulikirimia Kanisa katika ulimwengu mamboleo, licha ya magumu na changamoto zinazoendelea kujitokeza.

Maadhimisho ya Sinodi hii yamekwenda sanjari na kumbu kumbu ya Jubilee ya Miaka hamsini ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican ulipozinduliwa; mwanzo wa Mwaka wa Imani, kwani Viongozi wa Kanisa waliotangulia walikumbusha kwamba, Uinjilishaji Mpya ni mchakato endelevu unaofanyiwa na Mama Kanisa, hasa tangu miaka hamsini iliyopita, wakati waamini wengi waliokuwa wamebahatika kusikia Habari Njema ya Wokovu ikitangazwa masikioni mwao walipoanza kukengeuka na kupoteza dira katika imani na maisha yao ya Kikristo.

Hii ndiyo changamoto iliyojitokeza kwa Mama Kanisa katika azma ya Uinjilishaji Mpya kwa kutambua kwamba, ni Yesu Kristo peke yake anayeweza kuzima kiu na matarajio ya watu wa nyakati hizi. Ujumbe wa Habari Njema, hauna budi kutangazwa kwa umakini mkubwa mintarafu hali za kijamii na kitamaduni za watu husika.

Baba Mtakatifu anasema, katika maadhimisho ya Sinodi ya Uinjilishaji Mpya, amejipatia utajiri mkubwa wa mawazo, tafakari, mapendekezo na changamoto zilizotolewa na Mababa wa Sinodi na kwa msaada wa Sekretarieti ya Sinodi pamoja na Wasaidizi wake wa karibu, atahakikisha kwamba anazifanyia kazi ili kuweza kulipatia Kanisa Waraka unaotoa muhtasari wa mchago huu wa Mababa wa Sinodi juu ya Uinjilishaji Mpya.

Tangu sasa anasema Baba Mtakatifu, changamoto kubwa iliyoko mbele ya Kanisa ni kuhakikisha kwamba, linajikita katika toba na wongofu wa ndani, ili kuleta mabadiliko katika maisha ya kiroho yanayopania kuyatakatifuza malimwengu. Hili ni jibu makini linalotolewa na Yesu Kristo kwa kuzingatia kweli, neema na sura yake ya Kibinadam na Kimungu inayodhihirisha kwamba, Fumbo la Mungu linalipita uwezo wa Mwanadamu.

Baba Mtakatifu anayaweka matunda yote ya Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu juu ya Uinjilishaji Mpya chini ya ulinzi na usimamizi wa Bikira Maria, Mama wa Uinjilishaji Mpya, ili aweze kuwasaidia waamini kumpeleka Kristo kwa watu wote wakiwa na moyo wa ujasiri na furaha.







All the contents on this site are copyrighted ©.