2012-10-29 07:29:01

Kardinali Pengo: Maadhimisho ya Sinodi ya Uinjilishaji Mpya kimekuwa ni kipindi cha: Sala, Tafakari na Uinjilishaji


Mababa wa Sinodi ya Maaskofu juu ya Uinjilishaji Mpya katika Ujumbe wao kwa Watu wa Mungu sehemu ya mwisho, wanaangalia utume na maisha ya Kanisa katika sehemu mbali mbali za dunia na kuwapatia neno la matumaini kwa ajili ya sehemu husika. RealAudioMP3

Wanawatia moyo Waamini kutoka Makanisa ya Mashariki ili waweze kutangaza Injili ya Kristo katika mazingira ya amani na uhuru wa kuabudu; kwa Kanisa Barani Afrika, wanawaalika kukoleza moyo na ari ya Uinjilishaji kwa njia ya utamadunisho ili imani iweze kuzama na kuota mizizi katika maisha ya waamini.

Mababa wa Sinodi katika Ujumbe wao wanazichangamotisha Serikali mbali mbali Barani Afrika kuzingatia misingi ya utawala bora, sheria, uhuru wa kuabudu, ili kuondokana na kinzani na vurugu za kidini, kisiasa na kikabila. Wakristo wanaoishi Amerika ya Kaskazini wanahimizwa kuiishi imani yao katika ulimwengu ambao watu wengi wamekengeuka na kuzama zaidi katika malimwengu; wajitahidi kutubu na kuongoka; waoneshe moyo wa ukarimu kwa wageni na wahamiaji.

Wakristo huko Amerika ya Kusini wanahimizwa na Mababa wa Sinodi katika ujumbe wao kuendeleza utume wa Kanisa kama sehemu ya mchakato wa kupambana na baa la umaskini na ongezeko la madhehebu na dini katika maeneo yao. Wakristo Barani Asia hata katika udogo wao kwa idadi wanaendelea kuhimizwa kuimaarisha imani yao kwa Kristo na Kanisa lake.

Mababa wa Sinodi wanawaangalisha Waamini Barani Ulaya kuwa makini zaidi ili wasimezwe na malimwengu, daima wawe mstari wa mbele kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu, wawe tayari kutafuta mafao ya wengi ndani ya Jamii. Matatizo na magumu wanayokabiliana nayo iwe ni changamoto ya kukuza na kuimarisha Imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Wakristo huko Oceania wanaalikwa kwa namna ya pekee, kushiriki katika mchakato mzima wa Uinjilishaji Mpya.

Kardinali Polycarp Pengo, Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM katika mahojiano na Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican anabainisha kwamba, Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu juu ya Uinjilishaji Mpya kama njia ya kutangaza Imani ya Kikristo, yamekuwa ni muda muafaka wa kusali, kutafakari na kushirikishana mang’amuzi mbali mbali katika maisha na utume wa Kanisa.

Kimekuwa ni kipindi cha neema, toba na wongofu wa ndani, kwani Mababa wa Sinodi wamepata nafasi ya kuweza kupembua kwa kina na mapana kuhusu: matatizo, changamoto na fursa mbali mbali ambazo zimejitokeza mintarafu azma ya Uinjilishaji Mpya unaogusa undani wa maisha na utume wa Kanisa katika Ulimwengu mamboleo.

Dhana ya Uinjilishaji Mpya inapania kwa namna ya pekee kabisa, kutangaza Imani ya Kristo na Kanisa lake kwa ari, nguvu na ujasiri mkubwa zaidi, daima wakiendelea kusoma alama za nyakati, changamoto iliyotolewa na Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, yapata miaka hamsini iliyopita, lakini ujumbe wake bado ni hai kabisa katika maisha na utume wa Kanisa katika ulimwengu mamboleo.

Vita, kinzani na migogoro ya kidini, kisiasa na kijamii ni matunda ya ubinafsi, tamaa ya mali na madaraka; uvunjaji wa haki msingi za binadamu, uhuru wa kuabudu pamoja na kutomheshimu binadamu na utu wake. Hili ni Fundisho kuu hata kwa nchi za Kiafrika kwamba: maadili, utu wema, na haki msingi za binadamu zinapaswa kushughulikiwa kikamilifu kwa ajili ya mafao ya wengi ndani ya Jamii, vinginevyo Bara la Afrika linaweza kujikita likiogelea katika hatari kubwa kwa sasa na kwa siku za baadaye.

Kardinali Pengo anasema, kwa hakika, maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu juu ya Uinjilishaji Mpya yamesaidia mchakato wake wa Kuinjilishwa na kwa sasa anajisikia kwamba, yuko tayari hata yeye kuendeleza dhamana ya Uinjilishaji Mpya inayokazia kwa namna ya pekee; toba, wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha. Ikumbukwe kwamba, maadhimisho ya Sinodi ni tukio la Kikanisa linaloishirikisha Familia ya Mungu katika ujumla wake.

Baada ya Sinodi, Waamini wanapaswa kufahamu yale yaliyozungumzwa na Mababa wa Sinodi, kuyasambaza ili ukweli huu uweze kuwafikia wengi zaidi pamoja na kuibua mbinu mkakati wa utekelezaji wake kwa ajili ya mafao na ustawi wa Kanisa katika ngazi mbali mbali.

Anawaalika Waamini na wote wenye mapenzi mema, kusoma kwa makini Ujumbe wa Mababa wa Sinodi juu ya Uinjilishaji Mpya ili waweze kuumwilisha katika uhalisia na vipaumbele vya maisha yao, wakati wanapoendelea kusubiri Waraka wa Baba Mtakatifu mara baada ya Sinodi ya Maaskofu juu ya Uinjilishaji Mpya kama njia ya kutangaza Imani ya Kikristo.








All the contents on this site are copyrighted ©.