2012-10-29 10:31:57

JIUNGENI NA CHUO KIKUU HURIA - PINDA


Waziri Mkuu Mizengo Pinda amewataka Watanzania wahakikishe kuwa wao wenyewe na watoto wao wanatumia fursa ya kudahiliwa kwenye Chuo Kikuu Huria badala ya kuendelea kusubiri mabweni yajengwe kwenye Vyuo Vikuu.

“Kama tutasubiri mashirika na taasisi za dini au watu binafsi wajenge vyuo vikuu vya mabweni, ni dhahiri wanafunzi wengi wasio na uwezo wa kulipia ada katika vyuo hivyo watasubiri kwa muda mrefu ili wadahiliwe au wakose kabisa nafasi kwenye Vyuo Vikuu,” alisema.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo Jumamosi, Oktoba 27, 2012, wakati akiwahutubia washiriki wa mahafali ya 20 ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) yaliyofanyika kwenye viwanja vya chuo hicho eneo la Bungo, wilayani Kibaha, Pwani.

Alisema kuwepo kwa Chuo Kikuu Huria kumetoa fursa ya kuongeza udahili wa wanafunzi kwenye vyuo vikuu kwa kiwango kikubwa kwa vile kinaweza kuchukua wanafunzi wengi kwa wakati mmoja.

“Napenda kuwasihi wananchi kujiunga na chuo hiki kutokana na ubora wa elimu inayotolewa pamoja na uhakika wa kuendelea na shughuli za kazi, ajira binafsi na kumwezesha mtu kukaa pamoja na familia,” alisema.

Waziri Mkuu aliahidi kufuatilia ombi la ujenzi wa barabara ya lami iendayo kwenye chuo hicho ambayo haizidi kilometa nne ili ikamilike mapema. Pia alimtaka Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa ashirikiane na Wakala wa Majengo (TBA) kuharakisha upatikanaji haraka wa majengo mikoani kwa taratibu zinazokubalika ili yasaidie kutatua tatizo la vituo vya kufundishia wataalamu mikoani.

Jumla ya wahitimu 2,787 walitunukiwa vyeti, stashahada, shahada za kwanza, na stashahada za juu katika fani za Sayansi ya Jamii, Ualimu, Elimu Maalum, Biashara na Fedha, Sayansi, Sheria, Uhasibu, Uchumi, Mazingira, Utalii, Masoko, Kiswahili, Utawala, Uandishi wa Habari na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano.

Miongoni mwa viongozi waliohitimu jana ni Mke wa Waziri Mkuu, Mama Tunu Pinda aliyehitimu Shahada ya Uongozi wa Biashara na Biashara ya Kimataifa (BBA – International Business). Wengine ni wakuu wa mikoa ya Shinyanga na Simiyu, Bw. Ali Nassoro Rufunga na Bw. Pascal Mabiti wakiwemo pia Mkuu wa Wilaya ya Wilaya ya Mbeya, Dk. Norman Sigalla na Mbunge wa Tandahimba, Bw. Juma Njwayo.

Akihojiwa na waandishi wa habari mara baada ya kupatiwa shahada yake, Mama Tunu Pinda alisema anawasihi wanawake wote wajiendeleze bila kujali wako kwenye nafasi ipi kwani elimu haina mwisho. “Umuhimu wa elimu hauangalii kama wewe ni mke wa kiongozi au la, elimu inawahusu watu wote!,” alisema.

Alisema mahafali hayo yamempa hamasa ya kusoma tena zaidi na zaidi kwani ameona wahitimu wengine wakipata shahada za juu zaidi. “Nimeona wenzagu wakipokea Ph.D zao nikasema mimi nina Bachelor tu, hapana. Lazima niende mbele zaidi,” alisema bila kufafanua kuwa atasomea fani gani.

Mapema, Mwenyekiti wa Baraza la Chuo hicho, Prof. Samwel Wangwe alisema Chuo hicho tayari kinashirikiana na vyuo vingine vya elimu ya juu vya umma hapa nchini kama SUA, MUHAS, DIT na CBE ili kuongeza udahili wa wanafunzi vyuoni.

Alisema chuo hicho kina mpango wa kutumia teknolojia ya habari na mawasiliano kwa kuchapisha vitabu vya kujisomea kwenye CD na DVD ili kupunguza gharama za uchapishaji wa vitabu.

Aliziomba wizara zenye majengo yasiyotumika huko mikoani ziyatoe kwa chuo hicho ili yafanyiwe ukarabati na yaweze kutumika kutoa elimu kwa wataalam wengi zaidi nchini.

Alitumia fursa hiyo kuiomba Wizara ya Ujenzi waiingize barabara iendayo stesheni ya Soga kupitia chuoni hapo katika mpango wake wa muda mfupi ili iwekewe lami na hivyo kurahisisha mawasiliano kwa wakazi wa eneo hilo.

Naye Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Prof. Tolly Mbwete alisema Chuo hicho kina eneo la ekari 105 na kwamba kinatarajia kuanza ujenzi wa majengo mawili kwa ajili ya madarasa na ofisi za chuo ambao utagharimu sh. bilioni 15/-.

Kuhusu changamoto zinazokikabili Chuo hicho, Prof. Mbwete alisema wanakabiliwa na changamoto ya uhaba wa rasilmali fedha, uhaba wa mabweni na uhaba wa wanataaluma. Aliomba wapatiwe fedha kwa ajili ya kuimarisha miundombinu yake. Aliomba kuwe na ushirikiano wa karibu zaidi na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma ili wapatiwe fedha za malimbikizo ya mishahara ya wafanyakazi wa Chuo hicho.








All the contents on this site are copyrighted ©.