Familia yote ya Mungu ina wajibu fungamanishi juu ya Uinjilishaji Mpya kama njia ya
kutangaza Imani ya Kikristo!
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, Jumapili, tarehe 28 Oktoba, 2012 aliungana
na Mababa wa Sinodi, Viongozi mbali mbali wa Kanisa pamoja na Waamini katika ujumla
wao, kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kufunga Sinodi ya Maaskofu juu
ya Uinjilishaji Mpya kama njia ya kutangaza Imani ya Kikristo.
Baba Mtakatifu
wakati wa mahubiri yake amekumbusha kwamba, Injili ya Marko, kimsingi ni hija ya imani
inayofuata nyayo za Yesu Kristo na kwamba, Mitume wa Yesu ndio wafuasi wa kwanza kugundua
njia hii, lakini walikuwepo na watu kama Bartimayo Kipofu, muujiza wa mwisho uliotendwa
na Yesu wakati akiwa njiani kuelekea Yesrusalem.
Kipofu huyu ni kielelezo
cha mtu anayehitaji huruma na msaada wa Mungu katika maisha yake, anatambua kwamba,
amepoteza uwezo wake wa kuona, lakini bado Imani yake ni hai kabisa ndiyo maana anataka
kukutana na Yesu, tukio ambalo lilimkirimia tena uwezo wake wa kuona na kumrudishia
utu wake uliokuwa umepotea kutokana na upofu wake, akawa tayari kumfuasa Kristo katika
mwanga wa Imani.
Baba Mtakatifu anasema kwamba, Bartimayo ni kielelezo cha
utajiri mkubwa wa imani ambayo mwamini anaweza kuupoteza katika hija ya maisha yake,
hii ndiyo changamoto ya Uinjilishaji Mpya, inayopania kutoa fursa mpya kwa Waamini
kuweza kukutana tena na Yesu Mwana wa Mungu katika hija ya maisha yao hapa duniani.
Waamini wanahimizwa kumtangaza Kristo kwa ari na nguvu mpya katika maeneo ambayo Imani
imefifia, moto unaoonesha uwepo wa Mungu unaanza kuzimika.
Uinjilishaji Mpya
ni dhana inayogusa maisha ya Kanisa zima, lakini kwa namna ya pekee, unaigusa Mihimili
ya Uinjilishaji inapotekeleza majukumu yake ya shughuli za kichungaji, inapaswa kuwasha
moto wa Roho Mtakatifu kwa waamini wanaoshiriki katika maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa:
kwa kulishwa na Neno la Mungu pamoja na Mkate wa uzima wa milele.
Baba Mtakatifu
anabainisha kwamba, Mababa wa Sinodi kwa namna ya pekee, wamekazia umuhimu wa Kanisa
kuwa na maandalizi makini kwa wakristo wanaopokea Sakramenti zinazomwingiza Mwamini
katika Ukristo, yaani Sakramenti ya Ubatizo, Kipaimara na Ekaristi Takatifu. Waamini
wajichotee huruma na upendo wa Mungu unaobubujika kutoka katika Sakramenti ya Upatanisho,
kwani ni Sakramenti inayomwonesha mwamini utakatifu wa maisha anaopaswa kuufuata katika
hija ya maisha yake na kwamba, Wadau wakuu wa Uinjilishaji ni Watakatifu wanaoendelea
kuzungumza lugha inayoeleweka na watu na kwa njia ya maisha na utume wao, wamwefanikiwa
kutangaza Injili ya Upendo wa Kristo.
Uinjilishaji Mpya ni dhamana inayokwenda
sanjari na Utangazaji wa Habari Njema kwa wale ambao bado hawajabahatika kumfahamu
Yesu Kristo Mkombozi wa Dunia. Mababa wa Sinodi wamebainisha kwamba, bado kuna umati
mkubwa wa watu wasiomfahamu bado Kristo kutoka sehemu mbali mbali za dunia, changamoto
ya kumwomwomba Roho Mtakatifu ili aweze kumasha ari na moyo wa Kimissionari, unaowajumuisha
viongozi wa Kanisa na Waamini katika ujumla wao.
Utandawazi ni dhana ambayo
imepelekea mwingiliano mkubwa wa watu kutoka sehemu mbali mbali za dunia, changamoto
kwa Mama Kanisa kuwainjilisha hata wale ambao walibahatika kusikia Injili ya Kristo
lakini leo hii wamemezwa na malimwengu, kwani hawa pia wanayo haki ya kumfahamu Kristo
na Kweli za Kiinjili. Familia yote ya Mungu inawajibu fungamanishi katika Uinjilishaji
Mpya.
Bado kuna umati mkubwa wa watu wanaotamani kupokea Sakramenti ya Ubatizo
na kwa njia hii, wanaweza kukutana na Yesu anayewasaidia kugundua ile furaha ya imani
yao, kiasi hata cha kuanza kushiriki katika maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa kwa ari
kubwa zaidi.
Zote hizi zinapaswa kuwa ni jitihada za Mama Kanisa zinazojionesha
katika dhana nzima ya utamadunisho, ili kweli imani iweze kuota mizizi yake katika
maisha na waamini, wakijenga na kudumisha utamaduni wa majadiliano na Mwenyezi Mungu
ili kukuza urafiki na Mungu ambaye kimsingi ni upendo. Juhudu hizi ziende sanjari
na mikakati mbali mbali ya shughuli za kichungaji kwa kukuza na kudumisha kipaji cha
ugunduzi, ili kuwasaidia waamini waliokengeuka kupata tena maana ya: maisha na furaha
ya kweli ambayo kimsingi ni kukutana na Mwenyezi Mungu. Hizi ndizo juhudi zinazofanywa
na Kanisa kwa kukuza na kudumisha majadiliano ya wale wasioamini pamoja na utume wa
Mabara.
Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, kwamba, juhudi
zote hizi zitazaa matunda yanayokusudiwa kwa kupata baraka na neema kutoka kwa Yesu
Kristo Mchungaji Mwema. Wainjilishaji Wapya ni waamini ambao wamegundua kwamba, wameponywa
na Mungu kwa njia ya Yesu, kutoka katika undani wa maisha yao.
Hata leo hii,
Mama Kanisa anamgeukia Yesu Kristo: Mkombozi wa binadamu na mwanga wa mataifa kwa
moyo wa furaha na shukrani. Ni mwaliko wa kujivika mwanga wa Ukweli na kuondokana
na giza ili kuweza kufanya tafakari ya kina kumhusu Mungu. Ndivyo Baba Mtakatifu Benedikto
wa kumi na sita, alivyohitimisha mahubiri yake wakati wa Ibada ya Misa Takatifu kwa
ajili ya kufunga Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu juu ya Uinjilishaji Mpya.