Marehemu Padre Salutaris Lucas Massawe kuzikwa Jimboni Iringa hapo tarehe 30 Oktoba
2012
Jimbo kuu la Dar es Salaam linapokea kwa majonzi na masikitiko makubwa habari za kifo
cha Padre Salutaris Luca Massawe, Mkuu wa Shirika la Waconsolata Tanzania, kilichotokea
hapo tarehe 25 Oktoba 2012 kwa kuzama baharini, eneo la Msalaba Mtakatifu, mjini Bagamoyo
nyakati za Alasiri na mwili wake kupatikana asubuhi tarehe 26 Oktoba 2012.
Kanisa
limempoteza kiongozi mahiri na mchapakazi aliyetekeleza kazi zake kwa ufanisi. Kabla
ya kuchaguliwa na Wanashirika wenzake hapo tarehe 7 Septemba 2011 kuliongoza Shirika
nchini Tanzania, alishiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa Jimbo Kuu
la Dar es Salaam.
Anakumbukwa sana kutokana na mchango wake wa ushauri katika
maboresho ya Taasisi ya Tumaini Media, ambayo iko chini ya Jimbo kuu la Dar es Salaam,
inayosimamia TV Tumaini, Radio Tumaini na Gazeti la Tumaini Letu. Alikwisha wahi kufanya
utume wake katika Kituo cha Sala cha Waconsolata kilichoko Bunju, nje kidogo ya Jiji
la Dar es Salaam.
Askofu Msaidizi Eusebius Nzigilwa wa Jimbo Kuu la Dar es
Salaam amesema kwamba, kifo cha Padre Salutaris Lucas Massawe kimeacha pengo kubwa,
ambalo halitakuwa rahisi kuweza kuzibika.Waamini wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam wanatarajiwa
kufanya Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumwombea Marehemu Padre Salutaris Massawe
tarehe 29 Oktoba 2012 kabla ya kusafirishwa kwenda Jimboni Iringa kwa mazishi yanayotarajiwa
kufanyika hapo siku ya Jumanne tarehe 30 Oktoba 2012, kwenye Makao Makuu ya Shirika
la Wamissionari wa Consolata nchini Tanzania.