2012-10-26 12:26:09

Mkuu wa Shirika la Waconsolata Tanzania afariki dunia!


Mheshimiwa Padre Salutaris Lucas Massawe, aliyekuwa mkuu wa Shirika la Wamissionari wa Consolata, nchini Tanzania, amefariki dunia baada ya kuzama na baadaye kufa maji mjini Bagamoyo waliokuwa wamekwenda na Wanashirika wenzake kwa mapumziko mafupi baada ya mkutano wa wakuu wa Shirika la Waconsolata Barani Afrika, uliokuwa unafanyika Bunju, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.

Akizungumza na Radio Vatican, Padre Tobias Oliveira, Katibu mkuu wa Shirika la Waconsolata anasema, Padre Salutaris Massawe alifariki dunia hapo Alhamisi, tarehe 25 Oktoba 2012 na mwili wake kupatikana asubuhi ya tarehe 26 Oktoba 2012 huko mjini Bagamoyo.

Marehemu Padre Salutaris Massawe alizaliwa kunako tarehe 8 Julai 1962, Jimbo Katoliki la Moshi. Alisoma shule ya Msingi Singachini kuanzia mwaka 1971 hadi mwaka 1978 na baadaye akaendelea na masomo yake ya Sekondari Maua Seminari kati ya Mwaka 1980 hadi mwaka 1985. Aliendelea na masomo ya Falsafa na Taalimungu kwenye Chuo cha Waconsolata kilichoko mjini Nairobi kuanzia mwaka 1985 hadi mwaka 1988.

Baada ya masomo na majiundo yake ya Kipadre, kunako tarehe 27 Juni 1993 alipewa daraja takatifu la Upadre na Askofu Amedeus Msarikie wa Jimbo la Moshi wakati huo. Alibahatika kufanya utume wake kama Mmissionari wa Shirika la Consolata nchini Ethiopia, Kenya, Tanzania na Italia. Kunako tarehe 7 Septemba 2011 alichaguliwa kuwa Mkuu wa Shirika la Waconsolata nchini Tanzania hadi alipofariki dunia hapo tarehe 25 Oktoba 2012.







All the contents on this site are copyrighted ©.