2012-10-26 07:37:05

Familia ni kitovu cha Uinjilishaji Mpya na Urithishaji wa Imani katika mchakato mzima wa kuyatakatifuza malimwengu!


Kardinali Giovanni Battista Re, Mwenyekiti mstaafu wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makleri katika maadhimisho ya Jubilee ya miaka hamsini ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican sanjari na Mwaka wa Imani uliotangazwa na kuzinduliwa na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, hivi karibuni anabainisha kwamba, Familia ni mahali pa kwanza kabisa ambapo waamini wanaweza kujifunza kumfahamu, kumpenda na kumtumikia Kristo katika hija ya maisha yao ya Kikristo.

Changamoto kubwa kwa sasa kwa upande wa Kanisa ni kuhakikisha kwamba, Familia inapewa kipaumbele cha kwanza katika mipango na mikakati ya shughuli za kichungaji katika maadhimisho ya Mwaka wa Imani, ili kuendelea kukazia changamoto iliyotolewa na Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican kwamba, Familia ni Kanisa dogo la nyumbani, ni shule ya utakatifu, haki na amani kama alivyokazia pia Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili wakati wa hija yake ya kichungaji nchini Tanzania.

Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, yawe ni chemchemi ya kujenga na kuimarisha utamaduni wa: kusikiliza, kujisomea, kulitafakari na hatimaye, kulimwlisha Neno la Mungu katika hija ya maisha ya waamini. Tunu hizi muhimu katika maisha ya waamini, zitawawezesha pia kujenga mazingira ya amani na utulivu wa ndani unaobubujika kutoka katika Neno la Mungu.

Mwaka wa Imani, uwe ni Mwaka unaowajengea waamini uwezo wa kufurahia imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, wakiwa tayari kuitolea ushuhuda katika uhalisia wa maisha yao sanjari na kuwamegea wengine zawadi hii kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayopokelewa kwa unyenyekevu mkubwa.

Kardinali Giovanni Battista Re anasema, Mwaka wa Imani uwe ni changamoto ya kukuza na kuimaarisha imani kwa Kristo na Kanisa lake kwa njia ya Sala, Maisha ya Kisakramenti, Tafakari ya Neno la Mungu na Matendo ya Huruma. Nyenzo kuu zinazoweza kuwasaidia waamini katika mchakato huu wa maisha ni: Biblia Takatifu, Katekesimu Mpya ya Kanisa Katoliki, Mafundisho Jamii ya Kanisa, Nyaraka za Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican pamoja na Mafundisho mbali mbali yanayotolewa na Viongozi wa Kanisa kwa ajili ya utume na maisha ya Kanisa mahalia.

Ushuhuda wa Imani kwa Kristo na Kanisa lake, licha ya kwanza kabisa kujikita katika maisha ya mwamini binafsi, lakini inapaswa kukumbuka kwamba, hili ni tendo la hadhara linalopaswa kutolewa na Jumuiya ya Waamini, ambao kimsingi wanafahamika kama Kanisa. Ushuhuda huu pia ujioneshe katika maisha ya: Kifamilia, Jumuiya Ndogo ndogo za Kikristo pamoja na Vyama vya Kitume.

Familia iwe ni kitovu cha Uinjilishaji na urithishaji wa imani ya Kanisa na kutokana na Familia, imara na thabiti, waamini walei wanaweza kutoka kifua mbele kuwainjilisha wengine katika sekta mbali mbali za maisha ya kijamii, kama sehemu ya mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wameliachia Kanisa urithi mkubwa ambao waamini na watu wote wenye mapenzi mema wanaalikwa kuugundua wakati huu Kanisa linapoadhimisha Jubilee ya miaka hamsini ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican.

Ni Mtaguso ambao umeacha Nyaraka kumi na sita zilizosheheni ari na mwelekeo mpya wa Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo. Umefika wakati wa kuzimwilisha hati hizi katika uhalisia wa maisha na utume wa Kanisa anasema Kardinali Giovanni Battista Re.







All the contents on this site are copyrighted ©.