2012-10-25 09:32:25

Changieni ujenzi wa Makanisa Mahalia kwa hali na mali, kama sehemu ya Uinjilishaji Mpya unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili!


Askofu Mkuu Protas Rugambwa, Katibu mkuu Msaidizi wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu ambaye pia ni Rais wa Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa, anawahimiza wanafunzi wanaosoma Roma kujenga na kudumisha mshikamano wa dhati kwa ajili ya mafao yao binafsi na nchi wanamotoka na kwamba, viongozi wa Kanisa na Serikali wanafurahi wanaposikia kwamba, wananchi wao wanaendelea kudumisha umoja na mshikamano wa kitaifa hata wanapokuwa ughaibuni. RealAudioMP3

Askofu mkuu Rugambwa anamshukuru Mwenyezi Mungu na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, kwa kumwaminisha kushiriki katika utume wa kuliongoza Kanisa la kiulimwengu. Hii ni sadaka kubwa kwa ajili ya sifa na utukufu wa Mungu pamoja na ustawi wa Kanisa la Kristo. Anasema, anaendelea kupata ushirikiano wa dhati na Maafisa wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu.

Kwa namna ya pekee, Askofu mkuu Rugambwa anawaalika wanafunzi wanaosoma mjini Roma pamoja na Familia ya Mungu katika ujumla wake, kuhakikisha kwamba, wanashiriki kikamilifu katika ujenzi wa Kanisa mahalia kwa mawazo, maneno na utekelezaji wa majukumu na wajibu wao kwa Kanisa. Anawaalika watanzania kwa namna ya pekee, kushiriki katika utoaji wa maoni yao yatakayoiwezesha Tanzania kupata Katiba Mpya, ambayo kimsingi ni Sheria Mama.

Anasema, hii pia ni sehemu ya Uinjilishaji Mpya unaopania kugusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Ni sauti ya kinabii inayopania kulinda na kudumisha mafao ya wengi ndani ya Jamii. Amewachangamotisha Watanzania wanaosoma na kuishi mjini Roma kupanga siku maalum kwa kushirikiana na Ubalozi wa Tanzania, ili waweze kupata nafasi ya kusikiliza juu ya mchakato wa ukusanyaji wa maoni kuhusu Katiba Mpya, ili nao waweze kuchangia wakitambua kwamba, huu ni wajibu wao msingi kama raia.







All the contents on this site are copyrighted ©.