"Vijana acheni ubinafsi, tabia ya kujikweza, wapenda makuu na kuabudiwa"
Ifuatayo ni hotuba ya Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania, katika ufunguzi wa Mkutano
mkuu wa nane wa UVCCM uliofanyika mjini Dodoma tarehe 23 Oktoba 2012.
Nakushukuru
sana Kaimu Mwenyekiti na viongozi wenzako wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa CCM kwa
kunialika kuja kujumuika nanyi katika ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Nane wa UVCCM.
Nawapongeza kwa maandalizi mazuri ya Mkutano wenu. Nyota njema huonekana asubuhi.
Bila ya shaka mambo yataenda vizuri na vijana watapata fursa ya kuchagua viongozi
wao wanaowataka wao kwa ajili yao na kwa maslahi ya Jumuiya yao na ya Chama cha Mapinduzi.
Ndugu Mwenyekiti; Ndugu Wajumbe; Katika Ibara ya 5 ya Katiba ya Chama
cha Mapinduzi imeelezwa kuwa malengo na madhumuni ya CCM ni: “Kushinda katika uchaguzi
wa Serikali Kuu na Mitaa, Tanzania Bara na Zanzibar ili kuunda na kushika Serikali
Kuu na Mitaa katika Jamhuri ya Muungano kwa upande mmoja na Zanzibar kwa upande wa
pili“…
Kwa mujibu wa Ibara hiyo basi, sisi katika Chama cha Mapinduzi tunataka
Mwenyekiti wa Kitongoji awe wa CCM, Mwenyekiti wa Mtaa au Kijiji awe wa CCM, Serikali
ya Mtaa au Kijiji iwe ya CCM, Diwani awe wa CCM, Halmashauri ya Wilaya au Mji iwe
ya CCM, Mbunge au Mwakilishi awe wa CCM, Rais wa Jamhuri ya Muungano na Rais wa Zanzibar
wawe wa CCM na Serikali zetu mbili ziwe za CCM.
Ndugu Mwenyekiti; Tunapozungumzia
Serikali tangu ngazi ya vitongoji mpaka taifa kuwa ni ya CCM, tunazungumzia kushinda
katika uchaguzi katika ngazi hizo. Tena basi katika mfumo wa demokrasia ya vyama
vingi tuna maana ya CCM kupigiwa kura nyingi zaidi na wananchi kuliko vyama vingine
vya siasa vitakavyoshiriki. Kama mjuavyo, idadi ya vyama vya siasa vyenye usajili
wa kudumu imefikia 20 pamoja na CCM.
Ndugu Mwenyekiti; Jumuiya za Chama
cha Mapinduzi zimeundwa kuisaidia CCM kukubalika na kuungwa mkono na wananchi. Kila
Jumuiya inapaswa kufanya kazi na makundi maalum katika jamii licha ya jukumu la jumla
kwa watu wote wa Tanzania. Jumuiya ya Vijana imekabidhiwa kufanya kazi hiyo miongoni
mwa vijana wa nchi hii popote walipo.
Ndugu wajumbe; Chama cha Mapinduzi
kinaitegemea Jumuiya yake hii kufanya kazi ya siasa miongoni mwa vijana wa Tanzania
kuwashawishi wakubali kuwa wanachama na wapenzi wa CCM. Na kubwa zaidi kuwafanya
vijana waunge mkono, wapiganie na kuwapigia kura wagombea wa Chama cha Mapinduzi nyakati
za uchaguzi. Kwa muhtasari nasema kuwa Chama cha Mapinduzi ni Chama cha siasa kilichoundwa
kwa ajili ya kukamata uongozi wa dola. Aidha, Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa CCM ni
chombo cha siasa kilichoundwa kukirahisishia na kukiwezesha Chama cha Mapinduzi kutimiza
malengo na madhumuni yake hayo kwa kupitia vijana.
Hayo ndiyo matumaini makubwa
na ya msingi zaidi kuliko yote ya Chama cha Mapinduzi kwa Jumuiya yake hii. Pili,
Jumuiya hii inalo jukumu la ulinzi na utetezi wa Chama cha Mapinduzi. Chama chetu
hakina walinzi wengine zaidi ya UVCCM. Kwa ajili ya kutimiza majukumu hayo mawili
hamna budi kujipanga vizuri kifikra na kimkakati kuijenga na kuiimarisha Jumuiya.
Safari hiyo inaanzia kwenye kupata uongozi ulio bora. Hii ndiyo fursa mliyonayo leo,
msiipoteze.
Kaimu Mwenyekiti; Ndugu Wajumbe; Hakikisheni kuwa mnapata
Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na safu ya viongozi wazuri ambao wataiongoza vyema Jumuiya
ya Umoja wa Vijana na kuiwezesha kutimiza ipasavyo malengo na madhumuni yake. Viongozi
watakaoongoza juhudi za kuendeleza, kutetea na kulinda maslahi ya Chama chetu kupitia
kwa vijana. Viongozi watakaoiwezesha CCM kupata ushindi wa kishindo katika uchaguzi
wa Serikali za Mitaa mwaka 2014 na Uchaguzi Mkuu mwaka 2015. Kumbukeni kuwa mnachagua
viongozi wa kuongoza Jumuiya yenu kwa miaka mitano ijayo. Mkifanya kosa sasa mtalijutia
kwa miaka mitano ijayo. Majuto ni mjukuu. Hivyo, hamna budi kuwa makini kwa kuwachagua
viongozi wanaofaa kupewa dhamana hiyo nzito. Kwa kuwa ninyi wenyewe mnajuana, natumaini
hamtafanya ajizi.
Chagueni viongozi wanaoijua na kuipenda Jumuiya na wenye
mapenzi ya dhati kwa Chama cha Mapinduzi. Viongozi waaminifu, waadilifu na wachapakazi
hodari. Watu mtakaokuwa nao wakati wa jua na mvua na kuwavusha kuwapeleka kwenye neema
na mafanikio. Chagueni watu kwa kufaa kwao na sio kwa urafiki wenu au kufadhiliana.
Jambo muhimu la kuzingatia msimchague mtu anayetoa rushwa, mtu anayewarubuni
kwa ahadi za uongo. Nawasihi vijana wakataeni watu hao, wanyimeni kura zenu. Anayetoa
rushwa na ahadi za uongo hafai, hana uwezo wa kuongoza, hafai kupewa nafasi ya uongozi.
Vijana lazima muongoze kukitoa Chama chetu kwenye taswira ya rushwa.
Ndugu
Wajumbe; Chagueni mtu anayeweza kuiongoza vyema Jumuiya ili itimize ipasavyo wajibu
na majukumu yake kwa maslahi ya vijana wa Tanzania. Chagueni mtu atakayewavuta vijana
wote wa mijini na vijijini, wasomi na wasio wasomi waitumainie UVCCM kama chombo chao,
kimbilio lao, nguzo yao, mpiganaji na mkombozi wao. Mtu atakayewaunganisha vijana
wa Tanzania badala ya kuwatenganisha. Na, mwisho mtu mtakayemchagua awe na uwezo wa
kuiimarisha Jumuiya yenu ili ipate mafanikio zaidi kuliko yaliyopatikana sasa.
Ndugu
Mwenyekiti; Ndugu Wajumbe; Mkimaliza uchaguzi jipangeni vizuri kutimiza wajibu
wenu kwa wanachama wenu, kwa Chama cha Mapinduzi chenye Jumuiya yake. Jengeni na
imarisheni Jumuiya yenu kwa kina, marefu na mapana yake. Kazi yenu ya awali katika
kufanya hayo ni kujenga umoja na mshikamano miongoni mwa viongozi na kati ya viongozi
na wanachama na miongoni mwa wanachama. Katika historia ya Chama chetu na mila na
desturi ya demokrasia ndani ya Chama, uchaguzi ndiyo njia tunayoitumia kupata viongozi.
Kwa kweli ni njia bora kuliko zote na haina badala yake. Lakini, ina hatari zake na
iliyo kubwa ni ile ya kusababisha mgawanyiko au hata mpasuko miongoni mwa wanaogombea,
wapenzi wao na miongoni mwa viongozi na wanachama wa Jumuiya, Chama na hata jamii.
Kwa
kutambua ukweli huo, ndiyo maana nawakumbusha kuwa mara unapomalizika uchaguzi, msisahau
kazi ya kuziba nyufa na migawanyiko iliyotokana na uchaguzi. Kazi hii muipe kipaumbele
cha juu ili mpate utulivu utakaowapa fursa ya kupanga na kutekeleza mipango ya kujenga
na kuimarisha Jumuiya.
Ndugu Mwenyekiti; Naomba mambo matatu kwenu.
La kwanza, msisahau msemo wa wahenga usemao “asiyekubali kushindwa si mshindani”.
Nafasi ya Mwenyekiti au Makamu Mwenyekiti ni moja na kwamba atashinda mmoja tu na
wawili hawatapata. Kila aliyegombea ana imani au anatumaini kuwa yeye atakuwa ndiyo
huyo mshindi. Lakini, atambue pia kuwa anaweza kuwa miongoni mwa wale wawili ambao
hawatabahatika. Ajiandae hivyo na wapenzi wake nao wajiandae hivyo pia. Bahati mbaya
sana wengi wetu tunaogombea na hata wanaotuunga mkono hatuko tayari kufikiria hivyo.
Tunafikiria kushinda tu na hivyo tunaposhindwa tunapata taabu kukubali ukweli huo
na wengine hufikia kufanya mambo yasiyostahili. Kukataa matokeo na baya zaidi kufanya
vurugu au kutishia au hata kuondoka kundini.
Ndugu Mwenyekiti; Napenda kutumia
nafasi hii kuomba (na hili ndilo ombi langu la pili), kuwa muwe na moyo wa ustahamilivu
na ukomavu wa kisiasa. Muwe na moyo mpana wa kukubali matokeo hata yale yasiyopendeza.
Lazima ukubali kuwa mmoja wenu tu atapata na wawili watakosa na kati ya hao unaweza
kuwa wewe wa kupata au kukosa. Kubali ukweli huo na songa mbele kujenga Jumuiya yako
na kupigania Chama chako kwa mapenzi yale yale yaliyokufanya ujitokeze kuomba kukitumikia.
Ndugu
Wajumbe; Mtu mwenye mapenzi ya dhati na Jumuiya yake na Chama chake hatanuna au
kufanya vitendo vya hujuma ati kwa sababu tu yeye kashindwa uchaguzi. Hataamua kuzamisha
au kuacha jahazi lizame kwa sababu hakuchaguliwa. Akifanya hivyo yeye si muumini
wa dhati, ni mwanachama cheo. Akikosa hana hamu tena na Chama chenu. Ninaposema
hayo, nisieleweke kuhalalisha watu kufanyiwa dhuluma au hata rushwa. Lakini hata
ikiwa hivyo zipo taratibu zake za kufuatwa.
Ndugu Mwenyekiti; Ombi langu
la tatu kwenu ni kuwataka nyote mtambue kuwa kugombea ni haki ya kila mwanachama wa
Jumuiya, tena ipo kwa mujibu wa Katiba ya Chama na Jumuiya. Kila baada ya miaka mitano
uchaguzi hufanyika, hivyo, hakuna sababu ya kumchukia mwanachama aliyejitokeza kugombea.
Pia si dhambi kwa mwanachama kumuunga mkono au kumpigania mgombea ye yote anayemuona
yeye anafaa. Ni haki yake ya msingi.
Ukimchukia au kumuona adui mtu aliyeamua
kugombea nafasi unayogombea au kutokukuunga mkono wewe katika uchaguzi na akamuunga
mkono mgombea mwenzako, unadhihirisha una upungufu mkubwa wa maadili ya kidemokrasia.
Siyo mtakuwa hamuwatendei haki wenzenu bali pia mtakuwa mnathibitisha kuwa hamtoshi.
Mnaonesha kuwa ni watu wabinafsi wa hali ya juu, wenye tabia ya kujikweza isivyostahili
na wapenda makuu na kuabudiwa.
Ndugu Wajumbe; Watu wa aina hiyo watakuwa
viongozi wa makundi na ni wenye kulipiza visasi. Na, kwa tabia hiyo ukishashindwa
au hata ukishinda, Chama au Jumuiya itakuwa na mifarakano na misuguano isiyoisha.
Narudia kuwaomba na kuwakumbusha kuwa lazima muoneshe ukomavu wa kisiasa, na kwa ajili
hiyo muwe wavumilivu na watulivu hata pale mambo yakienda msivyotaka yawe.
Uchaguzi
ukiisha nyote mshikamane na mshirikiane kujenga Jumuiya yenu. Wale watakaoshinda
ndiyo waongoze njia kuwajumuisha wenzao. Mkishinda, msigeuze Jumuiya mali ya walioshinda.
Hii ni Jumuiya ya wote, walioshinda na walioshindwa. Msiwatenge, hawana Jumuiya yao
nyingine. Na, watakaoshindwa wawe mfano wa kuwa tayari kufanya kazi na wenzao.
Tukumbuke rai ya wahenga “yaliyopita si ndwele tugange yaliyopo na yajayo”
Kaimu
Mwenyekiti; Ndugu Wajumbe; Mkiziyangatia hayo, naamini mtatoka kwenye uchaguzi
huu mkiwa na nguvu mpya, ari mpya na kasi mpya ya kutimiza wajibu wa Jumuiya ya Umoja
wa Vijana wa CCM. Moja ya jukumu la msingi la UVCCM ni kufanya kazi ya siasa miongoni
mwa vijana wana-CCM na hasa wasiokuwa wana-CCM. Lengo likiwa kuwafanya wakubali kuiunga
mkono CCM. Kwa ajili hiyo, ningependa kuona Jumuiya yetu inajishughulisha zaidi na
changamoto zinazowakabili vijana wa Tanzania. Napenda kuona UVCCM mkiwa mstari
wa mbele kutambua na kuwasemea vijana mashuleni na vyuoni kwa matatizo na changamoto
zinazowakabili. Napenda kuona UVCCM ikiwa mstari wa mbele kuwasemea na kuwatetea
vijana wamachinga wapatiwe maeneo mazuri ya kufanyia kazi.
Napenda kuona
Umoja wa Vijana wa CCM ukiwasaidia vijana wasanii kuendeleza vipaji vyao na kuwapigania
wapate malipo ya haki kwa kazi zao wazifanyazo. Napenda kuona UVCCM wakiwa mstari
wa mbele kuendeleza vipaji vya michezo ya vijana na kuwa karibu na vijana wana michezo.
Aidha, napenda kuona Umoja wa Vijana ukijihusisha na masuala ya ajira kwa vijana.
Wasemeeni kwa sauti kubwa lakini pia wasaidieni pale mnapoweza wapate ajira. Wasemeeni
wanaotaka kujiajiri ili waweze kusaidiwa kujiajiri. Wasaidieni kwa kadri muwezavyo
vijana wanaotaka kujiajiri waweze kutimiza ndoto zao.
Ndugu Mwenyekiti; Ndugu
Wajumbe; Sina budi kutoa pongezi kwako na viongozi wenzako kwa kazi kubwa na nzuri
mliyoifanya na mnayoendelea kuifanya ya kuwawezesha vijana kupitia Tanzania Youth
Microfinance (TYM). Vijana wengi wamekuwa wananufaika kupitia SACCOS zao na vikundi
vyao vya uzalishaji mali na huduma. Endelezeni juhudi zenu hizo mpaka TYM siku moja
ije iwe Benki ya kutumainiwa siyo tu na vijana bali na watu wote. Mimi nawahakikishia
kuendelea kuwaunga mkono kwangu na msaada wangu nitakaojaliwa. Nawaomba pia muendelee
kuwahamiza vijana kujiunga na kuanzisha SACCOS. Ni mkombozi wao katika jitihada zao
za kujikwamua kimaisha kama ilivyo kwa Watanzania wote.
Ndugu Mwenyekiti; Ndugu
Wajumbe; Napenda kutumia nafasi hii kutoa pongezi maalum kwa uongozi wa Umoja wa
Vijana unaomaliza muda wake kwa kazi kubwa na nzuri mliyoifanya ya kuijengea Jumuiya
yenu uwezo wa kujitegemea. Nafurahi kwamba mmeendeleza kazi iliyoanzishwa na uongozi
uliowatangulia wa ujenzi wa jengo la kitega uchumi. Jengo sasa linaelekea kukamilika.
Tena linapendeza sana na kumfanya Baba yenu CCM kuona fahari ya mafanikio yenu. Si
hivyo tu mmempa baba changamoto ya kufikiria urefu na ubora wa majengo itakayoamua
kujenga. Wakati nawapongeza kwa mafanikio haya, nawaomba muendeleze maradufu juhudi
za uwekezaji. Fursa mnazo nyingi zitumieni.
Ndugu Wajumbe; Inatia moyo
kuona kuwa katika miaka mitano iliyopita, Jumuiya imezidi kuimarika na uwezo wa kiutendaji
unaongezeka. Vilevile Jumuiya inazidi kupata umaarufu na kupendwa na vijana wengi
zaidi kuliko ilivyokuwa awali. Wanachama wapya wameongezeka sana. Siku hizi wasomi
wengi wanajitokeza kuwa wanachama wa Jumuiya yenu na kuomba uongozi. Kwa kweli napata
faraja kwamba hatma ya CCM ina matumaini.
Kilicho muhimu sasa ni kuimarisha
safu ya uongozi wa vijana kwa kuwapatia mafunzo. Bahati nzuri Chuo cha Ihemi kipo.
Nimezungumza na Katibu Mkuu Martin Shigela kuwa tengenezeni mpango kabambe wa kukarabati
chuo na kukipanua. Nimemhakikishia kuwa nitawatafutia uwezo wa kufanya hivyo. Nataka
Chuo cha Ihemi kiwe ndicho Chuo cha CCM na Jumuiya zake kwa ajili ya kutayarisha makada.
Pia, kiwe kitovu cha kutoa mafunzo kwa viongozi wa Chama na Jumuiya zake.
Ndugu
Mwenyekiti; Chama kimeunda Jumuiya ya Vijana kuwa kama kikosi chake cha dafrau
cha kuondoa vizuizi na kusafisha njia kwa CCM kupita na kupata ushindi. Tunategemea
viongozi na wanachama wa UVCCM kukisemea, kukitetea na kukipigania Chama cha Mapinduzi
kwa kauli zenu na matendo yenu. Hatutegemei muwe tofauti. Naomba uongozi mpya muyazingatie
haya. Muangalie wenzenu walifanikiwa wapi na walikosea wapi. Imarisheni na endelezeni
mafanikio yaliyopatikana na sahihisheni kasoro zilizojitokeza. Anzeni ukurasa mpya
wa kujenga na kuimarisha UVCCM.
Ndugu Mwenyekiti; Kabla sijamaliza hotuba
yangu napenda kutoa rai moja kwenu. Nawaomba mhimize viongozi na wanachama wenu wajitokeze
kwa wingi kutoa maoni yao kwa Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba watakapotembelea
maeneo yao. Pia na nyie kaeni chini kama Umoja wa Vijana toeni mapendekezo yenu.
Kilio kina mwenyewe. Mambo ya vijana wenyewe vijana. Hii ni fursa adimu na adhimu
kwa vijana, kusema yao wanayoyataka yawemo katika Katiba yao. Wahamasisheni vijana
wajitokeze kwa wingi kutoa maoni yao na nyie toeni yenu. Huu ndio wakati wake.
Kaimu
Mwenyekiti; Ndugu Wajumbe; Natambua kwamba wengi wenu hivi sasa mnawaza kuhusu
uchaguzi, hivyo kila ninavyoendelea kusema mnasema mioyoni huyu mzee atamaliza lini
tumalize kazi. Naona sasa nimalize kwa kusema tena kwamba nawashukuru kwa kunialika.
Sisi katika CCM tunayo matumaini na matarajio makubwa kwenu kwani tunajua mmelelewa
vizuri katika Chama hiki chenye historia kubwa na chenye dhamana kubwa ya uongozi
wa nchi yetu. Tunategemea mtaupa uzito unaostahili uchaguzi wenu ili tupate viongozi
bora.
Hivyo nawaomba mtumie fursa ya Mkutano Mkuu huu wa Nane wa Taifa kuchagua
Viongozi wa Jumuiya watakaokidhi matumaini yetu na yenu ya kutekeleza majukumu ya
UVCCM na ya Chama cha Mapinduzi.
Baada ya kusema hayo, kwa heshima kubwa
natamka kuwa Mkutano Mkuu wa Nane wa UVCCM umefunguliwa rasmi. Nawatakia Mkutano mwema
na uchaguzi mwema wenye mafanikio tele.