2012-10-24 14:51:33

SIKU YA UMOJA WA MATAIFA, TAREHE 24 OKTOBA 2012


Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Ban Ki-Moon katika maadhimisho ya Siku ya Umoja wa Mataifa, inayoadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 24 Oktoba anabainisha kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inaendelea kuogelea katika dimbwi kubwa la ukosefu wa usalama, mabadiliko na athari za kipindi cha mpito.

Vurugu zinaendelea kuongezeka sehemu mbali mbali za dunia, pengo kati ya maskini na matajiri linazidi kupanuka kila kukicha na baadhi ya watu kukosa fadhila ya uvumilivu kati ya mambo ambayo yanaendelea kutoa changamoto kwa Jumuiya ya Kimataifa na kwa Serikali zake. Kutokana na changamoto kama hizi, Umoja wa Mataifa hauna budi kusimama kidete kulinda na kudumisha misingi ya haki, maendeleo, haki msingi za binadamu, utawala wa sheria pamoja na kuwajengea uwezo wanawake na vijana ili waweze kushiriki kikamilifu katika maisha ya kijamii.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anakiri kwamba, kumekuwepo na maendeleo makubwa katika baadhi ya maeneo yaliyotajwa hapo juu. Tangu mwaka 2000, kiwango cha umaskini duniani kimepunguzwa kwa kiasi kikubwa. Nchi nyingi duniani zinaendelea kufanya mchakato wa demokrasia, kuna dalili za kukua kwa uchumi hasa katika nchi changa zaidi duniani.

Umefika wakati kwa Jumuiya ya Kimataifa katika ujumla wake, kuwa na ari kubwa zaidi katika utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Millenia ifikapo mwaka 2015 pamoja na kubuni mikakati ya maendeleo inayotekelezeka baada ya mwaka 2015. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuendelea kupambana na tabia ya vurugu, kuwaokoa waathirika wa vita na kinzani za kisiasa na kijamii, ili hatimaye, kujenga na kuimarisha amani ya kudumu.

Bwana Ban Ki-Moon anasema kwamba, Umoja wa Mataifa si jukwaa la kuwakutanisha Wanadiplomasia, bali ni mahali pa kujenga na kudumisha misingi ya amani, maboresho ya huduma ya afya kwa Jamii; uwanja wa upendo na mshikamano kwa ajili ya kuwasaidia wakimbizi; watetezi wa haki msingi za binadamu wanaopania kuhakikisha kwamba, tunu hizi zinakuwa ni mwanga katika maisha ya Jumuiya ya Kimataifa.

Ili kutekeleza wajibu huu nyeti kwa Jumuiya ya Kimataifa, Umoja wa Mataifa unashirikiana na wadau mbali mbali yakiwemo: Mashirika Yasio ya Kiserikali, Wanasayansi, Wasomi, Viongozi wa Kidini, Wafanyabiashara na wananchi katika ujumla wao. Hakuna kiongozi, nchi au taasisi inayoweza kujitosheleza kwa kila jambo, lakini kila mtu anaweza kutekeleza walau kiasi cha wajibu wake.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anasema kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inapoadhimisha Siku ya Umoja wa Mataifa ni wajibu wake kukumbuka na kutekeleza kwa dhati ile dhamana yao kama mtu binafsi au Jamii katika ujumla wake yale Malengo yaliyobainishwa kwenye Katiba ya Umoja wa Mataifa, kama sehemu ya ujenzi wa dunia iliyo nzuri zaidi kwa ajili ya wengi.







All the contents on this site are copyrighted ©.